Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
WAUMINI wa Kikristo pamoja na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania(KKKT), Ushirika wa Makedonia Mjimwema Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria,wametakiwa kutumia ipasavyo talanta walizobarikiwa na Mungu, kwa kuzingatia wema na uaminifu kwa kadri ya uwezo wa kila mmoja.
Wito huo umetolewa Mei 3,2026 na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Makedonia Mjimwema, Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Emmanuel Muhangwa, wakati wa ibada ya Jumapili iliyokwenda sambamba na ibada ya kuwaingiza kazini viongozi wa idara mbalimbali wa ushirika huo waliochaguliwa kulitumikia kanisa kwa kipindi cha miaka minne ijayo,iliofanyika kanisani hapo.
Akihubiri, Mch.Muhangwa,amesisitiza kuwa kila muumini anapaswa kutumia talanta alizopewa kwa wema na uaminifu, akibainisha kuwa changamoto kubwa kwa wengi ni kukosa uaminifu licha ya kuwa na uwezo wa kufanya mema.
Ametolea mfano kutoka katika Maandiko Matakatifu, kitabu cha Mathayo 25:20–21, kinachoeleza juu ya mtumwa aliyepokea talanta tano na kuzizalisha nyingine tano, na kusifiwa na bwana wake kwa kuwa mwema na mwaminifu.
Aidha,amekumbusha kuwa watumishi wa Mungu walioteuliwa wanapaswa kuwa waaminifu katika majukumu yao, akirejea pia Mathayo 25:26 inayoonya dhidi ya kuwa watumwa wabaya na walegevu.
“Mungu anatuita tumuabudu katika roho na kweli, pamoja na kumtolea kwa moyo wa hiari, ikiwemo kushiriki katika ujenzi wa kanisa,”amesema Mch.Mugangwa na kuongeza:
“Mungu anamjua kila mtu alivyo, hivyo kila mmoja anapaswa kumtumikia kwa uaminifu, kutumia rasilimali na mali alizonazo kwa kumtukuza Mungu, na kutekeleza wajibu wake ipasavyo,”.
Mch.Muhangwa ameonya kuwa talanta isipotumika ipasavyo inaweza kunyang’anywa, akinukuu maandiko yanayosema talanta hupewa zaidi yule anayeitumia vizuri.
Sanjari na hayo amewataka viongozi kuepuka kiburi,kujiinua na kujikweza, badala yake wawe wanyenyekevu na watii,kufanya maombi na kusikiliza sauti ya Mungu pamoja na kuwaambia watu ukweli.
Huku amewasisitiza waumini kutokuwa walegevu na kuishi maisha ya faida, kuwa waaminifu na kuwapa ushirikiano viongozi hao.

More Stories
Waandishi 3,357 wapata Ithibati kupitia mfumo maalum
Samia atoa bil 20,waandaji maudhui wanufaika
Waandishi 3,357 wapata ithibati kupitia mfumo wa Tai Habari