May 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia atoa bil 20,waandaji maudhui wanufaika

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda amesema Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa kushirikiana na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, zitahakikisha zinawawezesha vijana wanaojiajiri katika sekta ya habari kwa kuwapa mitaji ya kukuza, kuendeleza na kuzalisha kazi zao katika ubora unaokidhi mahitaji ya soko kupitia mikopo yenye masharti nafuu.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Makonda amesema katika kutekeleza hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa Shilingi bilioni 20 kwa ajili ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 2 tayari zimetolewa kwa ajili ya mikopo kwa Watengeneza Maudhui Mtandaoni (content creators).

Amesema fedha hizo zinalenga kuwasaidia Watengeneza Maudhui kupata vitendea kazi na kuongeza uzalishaji wa kazi zao.

Hatua hiyo inatajwa kuwa mkombozi kwa vijana wanaojiajiri katika sekta ya habari na ubunifu, kwani inafungua fursa mpya za upatikanaji wa mitaji, vifaa vya kisasa na kuongeza uzalishaji wa maudhui yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa.

“Fedha hizi zinalenga kuwawezesha Watengeneza Maudhui kupata vitendea kazi, kuboresha ubora wa kazi zao na kuongeza ushindani katika soko la kidijitali,” alisema Mhe. Makonda.

Alisema hatua hiyo inaashiria mabadiliko ya kifikra katika namna Serikali inavyotambua na kuwekeza katika kundi la vijana wabunifu, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikua kwa kasi bila mifumo madhubuti ya kulisimamia na kulikuza.

“Huu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika ubunifu wa vijana na uchumi wa kidijitali, unaolenga kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania,” aliongeza.

Kwa mujibu wa wadau wa sekta hiyo, upatikanaji wa mitaji ni changamoto kubwa inayokwamisha ukuaji wa maudhui ya kidijitali, hivyo hatua hiyo ya Serikali inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa kazi bora, kukuza vipato na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha ubunifu wa maudhui katika ukanda wa Afrika Mashariki.