May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wauguzi wakumbhushwa kutumia lugha nzuri

Na. WAMJW, TimesMajira Online, Arusha

WAUGUZI na wakunga nchini wametakiwa kutumia lugha nzuri wanapokuwa wanahudumia wagonjwa kwani kwa kutofanya hivyo ni kinyume na maadili na miiko ya kazi zao.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ziada Sellah wakati akiongea na Wauguzi waliopo hospitali ya Rufaa Mkoa wa Arusha-Mount Meru.

Ziada amesema, wapo baadhi ya wauguzi au wakunga hutumia lugha chafu kwa wagonjwa na mara nyingine kuomba au kupokea pesa kutoka kwa wagonjwa pindi wanapofika kupata huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

“Vitendo hivi ni kinyume na maadili na miiko ya kazi yetu kwani katika viapo vya utumishi mliapa kuwatumikia na kuwahudumia wagonjwa kwa moyo na upendo, hivyo hakikisheni mnatimiza viapo vyenu,” amesema Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, Ziada amewapongeza wauguzi wote kwa kupambana vyema katika janga la Covid-19, kwani kipindi kile walisimama mstari wa mbele na kupambana na ugonjwa huo kwani ugonjwa huo ni mpya na hauna chanjo wala tiba.

“Niwapongeze sana kwa mapambano dhidhi ya ugonjwa huo ambao uliikumba dunia na nchi yetu, licha ya mazingira hatarishi lakini mliweza kupambana na hatimaye ugonjwa kuondoka hapa nchini,” amesema.

Amewataka wauguzi hao kutambua thamani yao kwani wao ni askari wa mbele katika vita vyote vya magonjwa kwa maana wao ndio wanampokea mgonjwa kwa mara ya kwanza anapofika kituoni na kumuhudumia kipindi chote anapokuwepo hospitalini hapo.

Katika ziara hiyo Mkurugenzi huyo amezindua kitabu kilichoitwa “COVID-19 VITA YA KARNE YA 19” ambacho kimeandikwa na Afisa Muuguzi Jane Barakululiza wa hospitali hiyo ambacho kinaongelea maisha kipindi cha Corona na hata baada ya Corona. Pia alitunuku zawadi kwa wauguzi waliopambana vyema katika kupambana na ugonjwa wa Corona.