May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi waombwa kuchangia damu kuokoa maisha ya mama na mtoto

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

IMEELEZWA kuwa uchangiaji wa damu umeendelea kuokoa maisha ya mama mjamzito na mtoto sababu zinazofanya wananchi wa Kanda ya Ziwa na Mkoa wa Mwanza kuombwa kuendelea kujitokeza kuchangia damu ili kuendelea kuokoa wakina mama hao.

Tafitiki zilizofanyika katika nchi nyingi za Afrika zinaonesha kuwa, vifo vya kina mama siyo tu vinachukua maisha ya wanawake lakini pia huathiri ustawi wa watoto na familia ambapo kwa kutambua umuhimu huo Wizara ya Afya imekuja na kampeni ya kukusanya damu nchi nzima yenye kauli mbiu ‘Damu salama uhai wa mama’ ambayo inahitimishwa leo.

Kampeni hiyo inalenga kukusanya damu kwa ajili ya kusaidia kundi hilo ambalo ni miongoni mwa makundi yenye uhitaji mkubwa wa damu.

Ofisa Uhamasishaji Damu Salama Kanda ya Ziwa, Bernadino Medaa ameuambia Mtandao huu kuwa, mbali na kuokoa maisha ya watu wengine pia uchangiaji damu unamfanya mtu apate thawabu na baraka kutoka kwa Mungu.

Pia inasaidia mtu kupata huduma ya kupima magonjwa mbalimbali bila gharama yoyote, hivyo ni vyema wananchi wakajitokeza katika kuchangia damu ili kunusuru watu wanaohitaji damu hasa wanawake wajawazito.

Amesema, uchangiaji wa damu mara kwa mara kunampa fursa mchangiaji kupewa kadi ambayo itamsaidia yeye au ndugu yake kupatiwa damu bila gharama yoyote endapo kama atakutana na tatizo la kuhitaji damu.

Ripoti ya Wizara ya Afya inaonesha kuna vifo 556 kwa vizazi hai 100,000 kama ilivyotolewa taarifa kwenye utafiti wa mwaka 2015 kutokana na changamoto za uzazi vifo hivyo ni asilimia 18 ya vifo vyote vya wanawake wenye umri kati ya miaka 15-49.

Hali ya vifo vinavyotokana na uzazi nchini bado kwa kiasi kikubwa vinachangiwa na changamoto ya upatikanaji wa damu salama kwa wakati moja ya tatu ya vifo vyote vya wajawazito hutokea kwa sababu ya kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua.