May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa USAID Tulonge Afya kunufaisha Manispaa za Musoma, Rorya

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

HALMASHAURI za Manispaa ya Musoma na Rorya mkoani Mara, zinatarajiwa kunufaika na mradi wa miaka mitano wa Tulonge Afya, unaolenga kutoa elimu katika jamii ili kubadili tabia hasi na hatimaye kuwa na afya bora kama inavyotakiwa.

Mradi huo unaotekelezwa na serikali kwa kushirikiana na Shirika lisiloluwa la kiserikali la FHI360 chini ya Asasi ya One World Sustainable Livelihood (OWSL) kwa ufadhili wa Shirika la misaada la kimarakeni la USAID pamoja na mambo mengine, utatoa elimu dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa pamoja na elimu ya afya ya uzazi kwa walengwa.

Akizungumza mjini hapa leo, kwenye mafunzo kwa akinamama juu ya umuhimu wa unyonyeshaji, Mratibu wa OWSL, Dkt. Theophil Kayombo amesema, katika utekelezaji wa mradi huo wanatarajia kuwafikia walengwa zaidi ya laki tatu katika halmashauri hizo mbili wengi wao wakiwa ni akinamama na vijana.

Amesema, asasi yake imemua kutekeleza mradi huo katika maneo hayo mkoani Mara kutokana na viashiria vya afya ya uzazi, mama na mtoto kuwa chini ikilinganishwa na halmashauri zingine ndani ya mkoa huo.

Hata hivyo amesema, njia mbalimbali zitatumika kuwafikia walengwa hao ikiwa ni pamoja na uundwaji wa vikundi,elimu kwa njia mbalimbali lengo likiwa ni kuwafikia walengwa katika makundi yao ili waweze kuelimika na kufuata kanuni bora za afya kama inavyoelekezwa na wataalam.

Mratibu wa uhamasishaji huduma za jamii kutoka ofisi ya mganga mkuu wa manispaa ya Musoma, Dkt. Magreth Shaku ameishukuru asasi hiyo kwa kuamua kutekeleza mradi huo ndani ya manispaa ya Musoma kwa maelezo kuwa mradi huo umekuja muda muafaka, hivyo utasaidia katika kuongeza uelewa wa jamii juu ya masula mbalimbali ya afya ikiwemo suala la kunyonyesha watoto hasa katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo mtoto anapozaliwa.

Dkt. Shaku amesema, suala la unyonyeshji wa watoto bado linakabaliwa na changamoto mbalimbali zinazopelekea akinamama kushindwa kunyonyesha kama inavyoshauriwa kitaalam hali ambayo kwa namna moja ama nyingine imekuwa ikileta changamoto katika suala zima la makuzi ya mtoto.

Alizitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na baadhi ya akinamama kukataa kunyonyesha watoto wao wakidai kuwa maziwa yao yataanguka pamoja na ushiriki hafifu wa akinababa kwenye suala zima la malezi ya mtoto.

Aliwataka akinamama kuhakikisha kuwa wananyonyesha watoto ipasavyo kwa maelezo kuwa mbali na unyonyeshaji kuwa na manufaa katika makuzi ya watoto lakini pia ni njia kuu mojawapo ya kumkinga mama dhidi ya ugonjwa wa saratani ya matiti.

Naye mratibu wa mradi huo, Cyprian Lungu, amesema mradi huo unalenga kuleta mabadiliko ya tabia kwa kupambana na tabia hasi katika jamii zinazozuia wanajamii kupata huduma bora za afya.

Amsema, akinamama watapata elimu juu ya namna wanavyotakiwa kujiandaa kiafya kabla na baada ya kujifungua pia namna bora ya kuwalea watoto wao katika umri wa chini ya miaka mitano jambo ambalo litasaidia kuwa na jamii iliyo bora.