May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wanawake hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya watoa msaada wa Kitanda

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

UMOJA wa watumishi wanawake katika hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya(MZRH)umetoa msaada wa kitanda cha kisasa kwa ajili ya upasuaji chenye thamani ya zaidi mil.37 ili kuweza kupunguza changamoto ya uhaba vitanda hospitalini hapo .

Akipokea kitanda hicho April 18,2024 Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Dkt.Godlove Mbwanji amesema kuwa wanawake hao wana fikra za mbali na kusema kuwa kitanda hicho kitapunguza changamoto za uhaba wa vitanda kwa ajili ya upasuaji.

“Mungu awabariki wote walioguswa kuchangia kitanda hiki lakini naomba nitoe wito kwa wadau wengine kujitokeza kutoa misaada kutokana na Hospitali yetu kuongeza idadi ya vyumba vya upasuaji hivyo bado tuna uhitaji mkubwa katika idara hii “amesema Dkt.Mbwanji.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mwenyekiti wa Umoja huo,Stellah Nkwama amesema lengo la kutoa msaada huo ni kuungana na wanawake wengine katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani hufanyika kila mwaka mwezi Machi.

“Tunatambua katika kada yetu kuna vitu vingi vinahitajika hivyo tukaona katika umoja wetu tujichangishe wenyewe fedha na kununua kitanda cha kisasa ambacho kitasaidia upasuaji wa aina zote ,ingawa bado mahitaji ya vitanda bado yanahitajika tukaona ni bora tutoe hata hiki kimoja tulichonacho wakati wadau wengine wanaendelea kujitokeza “amesema .

Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa wanawake ambaye pia ni Mkurugenzi wa Rasilimali watu ,Miriam Msalale amesema wamechangishana ili kupata fedha hizo kupitia mishahara,posho na biashara zao kutokana na umuhimu wa kitanda hicho.

Mkuu wa ldara ya Upasuaji Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ,Dkt.Lazaro Mboma amesema kitanda hicho cha kisasa kitaongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Naye Mkuu wa kitengo cha mifupa Dkt. John Mbanga amesema awali katika upasuaji kulikuwa kunahitaji watu zaidi ya wanne kwa upasuaji wa mtu mmoja lakini kupitia kitanda hicho daktari mmoja anaweza kufanya upasuaji.

“Hiki ni kitanda kipya na cha kisasa zaidi ambacho kitatuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika kazi zetu za kuhudumia wagonjwa wakati wa upasuaji,” amesema Dkt.Mbanga.

Mhandisi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya,Salum Kashinje amesema kitanda hicho kimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa ambapo matengenezo yake ni rahisi ukilinganisha na vitanda vya awali na kufanya huduma kuendelea kuboreshwa zaidi .

Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya imekuwa ikiboresha huduma zake siku hadi siku na kuifanya kuwa kimbilio katika mikoa ya Nyanda za Juu na nchi za Kusini.