
Na Israel Mwaisaka, Rukwa
Watumishi wa Umma wametakiwa kuujua na kuukubali mfumo wa PEPMIS kwa kuhakikisha wanautumia kwa kujaza taarifa zao za kiutendaji kwani mfumo huo ndiyo suluhisho la changamoto mbalimbali ikiwemo ya upandaji wa madaraja.
Wito huo umetolewa Jana na kaimu Katibu tawala wa mkoa Rukwa Rock Msalangi kwenye maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma iliyofanyika kata ya Kirando wilayani Nkasi ambapo amedai mfumo wa PEPMIS ni mbadala wa OPRAS katika kupima utendaji wa Kila mtumishi na kuwezesha kuufahamu uwezo wa Kila mtumishi kwa wakati.
Amesema kuwa mfumo huo wa PEPMIS ni rahisi sana kwa maana ni wa kidigitali hivyo haoni sababu ya Watumishi kushindwa kuutumia katika Kutoa taarifa zao na kuwezesha kuufahamu utendaji wao wa kazi.
Msalangi amefafanua kuwa hivi Sasa kipimo kikuu Cha utendaji kwa Watumishi wa Umma ni mfumo huo na kuwa na hata uteuzi wa nafasi mbalimbali za kiutendaji serikalini kwanza wanauangalia mfumo huo wa PEPMIS,kwani hata kama utakua bora sana kiutendaji lakini ukashindwa kujaza taarifa zako kwenye PEPMIS utendaji huo haujulikani.
Pia katika maadhimisho hayo watumishi wamekumbushwa kujiheshimu ikiwa ni pamoja na kuvaa mavazi yenye staha wawapo kazini na hata nje ya kazi kwani wao ni mfano katika jamii na wanaiwakilisha Serikali hivyo wawe ni mfano wa kuigwa na Kila Mtu katika jamii wanayoishi.
Na pia wametakiwa kujiepusha na matendo yoyote mabaya badala yake ni kujibidiisha katika kufanya kazi ili jamii inayohudumiwa iridhike na sifa nzuri ziende kwa Serikali ambayo ndiyo yenye jukumu kubwa la kuwahudumia Wananchi .
Katika maadhimisho hayo ya utumishi wa Umma yalienda sambamba na kusikiliza kero za baadhi ya Watumishi ambapo baadhi ya kero hizo zilitafutiwa ufumbuzi wa papo hapo na nyingine zilibebwa kwa ajili ya utatuzi Zaidi.
Awali Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Nkasi Misheck Chapewa alidai kuwa Watumishi 391 walipangwa kupanda vyeo lakini 368 ndiyo waliopanda vyeo na 23 hawakupanda baada ya kutotimiza vigezo, Watumishi 45 walitakiwa kubadilishiwa muundo wao wa kiutumishi lakini waliofanikiwa ni 23 tu na moja ya kikwazo kikuu kwa baadhi Yao kutofanikiwa ni kutojaza mfumo wa PEPMIS sawa sawa.

More Stories
Wasimamizi wa miradi ya maendeleo Rukwa wajengewa uwezo na Takukuru kuokoa Fedha za Umma
Washindi ‘kila muamala bao la ushindi’ waendelea kupeta
TMA yaeleza faida taarifa hali ya hewa