
Na Mwandishi wetu,Rukwa
Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa leo, Juni 26, 2026, wamepatiwa mafunzo kuhusu UKIMWI, magonjwa sugu yasiyoambukiza, pamoja na masuala ya jinsia, unyanyapaa na ukatili mahali pa kazi. Mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa wa watumishi kuhusu namna ya kulinda afya zao na kujenga mazingira salama na yenye usawa kazini.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi.Daudi Sebyiga, amewataka watumishi kuwa mfano bora katika kuzingatia afya zao kwa kufuata kanuni za kinga na uchunguzi wa mara kwa mara. Amesema afya njema ni msingi wa kuongeza ufanisi, tija na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Mkoa wa Rukwa Donald Nsokko amesema watumishi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiafya zinazohitaji elimu na ushauri wa wataalamu. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha afya za mwili na akili, hivyo kuongeza ari ya kufanya kazi na kupunguza changamoto zinazoweza kuathiri utendaji wao.
Aidha, amebainisha kuwa mafunzo hayo pia yamejikita katika kushughulikia changamoto za kisaikolojia na kijamii zinazoweza kujitokeza mahali pa kazi, ikiwemo rushwa ya ngono, upendeleo, ubaguzi na vitendo vingine vinavyokiuka maadili ya utumishi wa umma na kuathiri haki za watumishi.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na Dkt.

Gibons Willy kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Rukwa ambaye ametoa elimu kuhusu kinga na udhibiti wa UKIMWI pamoja na magonjwa sugu yasiyoambukiza. Washiriki wamehimizwa kuzingatia mtindo bora wa maisha, kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kutumia huduma za ushauri nasaha pale inapohitajika.
Naye Mariam Kimashi, Afisa Maendeleo ya Jamii, ametoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na unyanyapaa mahali pa kazi.

Amesema vitendo hivyo hudhoofisha utendaji kazi, kuvunja mshikamano miongoni mwa watumishi na kukiuka haki za msingi za binadamu, hivyo amesisitiza umuhimu wa kujenga mazingira ya kazi yenye heshima, usawa na uwajibikaji kwa wote.



More Stories
Serikali kuendeleza ujenzi Miundombinu ya Elimu Nanyumbu
Chadema ni kiwanda Cha kutengeneza chuki-UVCCM
FCC yapongezwa kwa kuimarisha vita dhidi ya bidhaa bandia