April 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu watakiwa kuilewa Dira

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOline,Arusha

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Hamza Johari amewataka watumishi wa ofisi yake pamoja na wadau wengine wa sheria kuhakikisha kuwa wanaisoma vyema Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 na kuielewa ipasavyo kwani ofisi yake inatakiwa kutekeleza Dira hiyo kwa asilimia zote.

Johari amesema hayo jijini hapa leo Aprili 27,2026 wakati akizungumza kwenye Baraza  la wafanyakazi wa Ofisi hiyo ambapo amesema ili dira hiyo iweze kunufaisha  jamii sekta ya sheria inatakiwa kila mmoja aweze kuzisimamia ipasavyo.

“Dira ya 2050 sisi ni washiriki tena wakubwa natumia jukwaa hili kuwahimiza kila mmoja aisome aielewe lakini pia muhakikishe kuwa mnawajibika ipasavyo kwenye masuala ya sheria”alisema.

Aidha aliwataka wafanyakazi wa Ofisi hiyo kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa kuzingatia malengo ya Ofisi.

“Malengo yetu pamoja na vipaumbele tulivyoweka kama Taasisi vinatakiwa kufanyiwa kazi kila kazi nzuri tunayoifanya kwa kushirikiana inaruhusu hata ongezeko kubwa la bajeti ya ofisi yetu,”alisema.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Rashid Kigalu amesema kuwa wao kama watumishi wa ofisi hiyo wanashukuru Ofisi yao kwa kuweza kuwapa fursa mbalimbali kama vile mafunzo Sekta ya Afya,pamoja na mafunzo ya ndani ya uwajibikaji wao.

Kigalu amesema  kuwa fursa hizo zimeweza kuruhusu uwajibikaji wa hali ya juu hali ambayo imeleta ongezeko kubwa la bajeti ya ofisi hiyo.