April 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afrika yatajwa kunufaika na mabilioni ya madini, endapo itaacha kuuza Malighafi Ghafi

Na Penina Malundo,Timesmajira

Nchi za Afrika zimetakiwa kuacha kuuza malighafi za madini na badala yake kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani ili kunufaisha wananchi na kukuza uchumi wa ndani.

Rai hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kikanda kuhusu matumizi ya madini muhimu kwa maendeleo ya viwanda vya kijani, lililofanyika katika makao makuu ya United Nations Economic Commission for Africa (UNECA) jijini Addis Ababa.

Dessalegn amesema licha ya Afrika kuwa na utajiri mkubwa wa madini muhimu kama cobalt, lithium, copper na manganese, bado wananchi wengi wanaishi katika umaskini kutokana na nchi nyingi kubaki katika kuuza malighafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani.

“Ni lazima Afrika iondoke katika nafasi ya chini ya mnyororo wa thamani na kuhakikisha madini yake yanachochea maendeleo ya viwanda na ustawi wa wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa ongezeko la mahitaji ya madini hayo duniani, hasa katika utengenezaji wa betri, magari ya umeme na nishati jadidifu, linatoa fursa kubwa kwa bara hilo ikiwa litabadilisha mkakati wake wa kiuchumi.

Aidha, Dessalegn amesisitiza umuhimu wa kuimarisha taasisi za usimamizi wa sekta ya madini ili kuhakikisha uwajibikaji, ulinzi wa mazingira na haki za wafanyakazi zinazingatiwa.

Akizungumzia ushirikiano wa kikanda, amesema matumizi bora ya fursa ya African Continental Free Trade Area (AfCFTA) yanaweza kusaidia Afrika kujenga mnyororo kamili wa thamani katika sekta ya madini na teknolojia ya kijani.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Tanzania, Msafiri Mbibo, amesema Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha wananchi kupitia sera za kuongeza thamani na uchimbaji unaozingatia mazingira.

“Tumejipanga kuhakikisha sekta ya madini inachangia zaidi ajira, kipato na maendeleo endelevu ya wananchi,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo, amesema Afrika inahitaji uongozi thabiti na sera madhubuti ili kusimamia vyema rasilimali zake na kufanikisha maendeleo jumuishi.

Kongamano hilo limewakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Afrika, likiwa na kaulimbiu inayohimiza bara hilo kuacha kuuza malighafi na kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani