May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto wawili wamefariki baada ya kuzama kwenye dimbwi la maji

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Watoto wawili wenye umri wa miaka 13 na 10 ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi Kitumba iliopo Kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza wamepoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu baada ya kuzama kwenye dimbwi la maji wakati wakiogelea.

Ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza lilipokea taarifa ya watoto wawili ambao ni Omary Denis mwenye umri miaka 13, mwanafunzi wa darasa la saba na Brayan Stephen mwenye miaka 10, mwanafunzi wa darasa la tatu wote walikuwa wakisoma shule ya msingi Kitumba kuwa wamezama kwenye dimbwi la maji wakati wanaogelea.

Akizungumza Aprili 24,2024 na waandishi wa habari mkoani hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 20,2024 majira ya saa 11 jioni katika kijiji cha Kitumba,Kata ya Kisesa, wilayani ya Magu.

Mutafungwa ameeleza kuwa baada ya jitihada za uokoaji kutoka kwa wananchi na wazazi wa watoto hao,waliwapeleka kituo cha afya Kisesa na baadae walifariki wakiwa wanapatiwa
matibabu kwenye kituo hicho.

Miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi huku
jeshi hilo likitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari ya hali ya hewa inayosababisha na
mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoani hapa kwa kutowaruhusu watoto kucheza kwenye mabwawa na mashimo yenye maji kwani ni hatari kwa usalama wao.

Huku akiwataka madereva wa vyombo vya moto pamoja na watembea kwa miguu kuchukua tahadhari ya kutokupita kwenye maeneo hatarishi ambayo yana historia ya kujaa maji na kufunika eneo la kupita mfano madaraja na
maeneo ya barabara yenye mkondo wa maji.