May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto watatu wa familia moja wafariki kwa kuuwawa na fisi

Na Esther Macha, TimesmajiraOnline, Mbeya

WATOTO watatu wa familia moja katika kitongoji cha Gengeni kilichopo kata ya Kambikatoto wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kuvamiwa na Kung’atwa wakiwa wamelala usiku wa manane huku wazazi wa watoto hao wakijeruhiwa vibaya.

Kwa Mujibu wa Kaimu Kamanda wa polisi Mkoani Mbeya ,Abdi Issango amesema kuwa tukio hilo limetokea April 7, mwaka huu majira ya usiku katika Kitongoji cha Gengeni kilichopo kata ya Kambikatoto tarafa ya kipembawe wilaya ya Chunya.

Kaimu Kamanda Issango amesema mnyama pori huyo aina ya fisi alivamia nyumba ya Shigela Ngasa (45)Mkazi wa Gengeni na kuwauwa kwa kuwang’ata watoto watatu wa familia hiyo ambao ni Samweli Shigela (05) Kasunzu Shigela (03)na Ngasa Shigela mwaka mmoja wote wakazi wa Gengeni.

Hata hivyo amesema kuwa katika tukio hilo fisi huyo aliwajeruhi wazazi wa watoto hao ambao ni Shigela Ngasa [baba] na mke wake aitwaye Limi Masanja (38)wote wakazi wa Gengeni.

Aidha Issango amesema baada ya tukio hilo Fisi huyo aliua kondoo wawili na kisha akakimbia uelekeo wa Hifadhi ya Rungwa eneo la Kambikatoto.

Amesema kuwa Fisi huyo aliweza kuingia ndani ya nyumba hiyo kutokana na nyumba hiyo kutokuwa na mlango na ipo jirani na pori la hifadhi ya Rungwa .

Hata hivyo amesema amesema majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Gasper – Itigi, Wilaya ya Manyoni, Mkoa wa Singida kwa matibabu zaidi.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa wanyama pori kutoka pori la akiba la Rungwa na wananchi wa Gengeni limefanikiwa kumuua Fisi huyo ambaye alikimbilia Porini na baadae kurudi tena Kijijini hapo na kuwawa.