April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto milioni 6.7 kupata chanjo ya polio

*Serikali yaanza kampeni  kuwakinga watoto kutoka mikoa saba ikiwemo ya Kanda ya Ziwa 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Zaidi ya watoto milioni 6.7,wenye umri chini ya miaka 10, kutoka mikoa saba ikiwemo ya Kanda ya Ziwa wanatarajiwa kupata chanjo ya matone ya kuwakinga na ugonjwa wa polio,kupitia kampeni maalumu  ilioanza Machi 24 hadi Machi 27,2026.

Kampeni hiyo ambayo inafanyika kwa siku nne katika mikoa ya Mwanza,Shinyanga,Geita,Simiyu,Mara,Singida na Tabora,ina lenga  kuhakikisha wanaimarisha kinga za watoto kutokana na uwepo wa taarifa za ugonjwa huo katika nchi jirani.

Akizungumza Machi 24,2026, katika uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo ya utoaji chanjo ya polio kwa mikoa saba ambayo Serikali imetoa kiasi cha bilioni 6 kwa ajili ya chanjo hiyo,iliofanyika Kisesa wilayani Magu,mkoani Mwanza,Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela,amesema wanaotoa chanjo hizo ili kuimarisha kinga za watoto hao na kuweza kukabiliana na ugonjwa wa polio ambao unaambukizwa kutokana na uchafu kama kinyesi.

Hivyo amewahimiza wazazi,walezi na wananchi kujitokeza kwa wingi kuanzia siku hiyo ya kwanza na wasisubili siku ya mwisho huku akiwahahikishia kuwa chanjo hiyo ni salama kwa afya ya mtoto.

“Niwasihi kushiriki katika kampeni hii,kwani Serikali imejipanga kuhakikisha inatoa kinga kwa watoto chini ya umri wa miaka 10 zaidi ya milioni 6.7,katika awamu hii ya kwanza kwa mikoa saba,kwa Mkoa wa Mwanza tunatarajia kuchanja watoto zaidi ya milioni 1.2.Pia mhakikishe wanapata chanjo ya pili ambayo itatolewa Mei 7 hadi 10,2026,usipokamilisha chanjo ya pili ndio yanaanza maneno kuwa chanjo hizo hazina ubora,”amesema Shigela na kuongeza:

“Tumepiga hatua kama nchi mgonjwa wa mwishoni alitokea miaka 30 iliopita mwaka 1996, zote hizo ni jitihada.Tumekuwa na mila na desturi za kubeza chanjo,tunaendesha kampeni ya chanjo wengine wanapeleka watoto,ina kuwepo kampeni hasi ya kusema ukichanja mtoto ina muathiri kwenye ukuaji,uzazi na mfumo wa fahamu,tusiruhusu kampeni hiyo hasi,”.

Mganga Mkuu wa Serikali,Dkt.Grace Magembe,amesema,katika mikoa hiyo yote wanazo timu takribani 14,000, ambazo zitatoa huduma hizo za chanjo,na ili wawafikie watoto wengi chanjo hizo zinatolewa katika vituo  vya tiba ikiwemo zahanati,vituo vya afya,hospitali za wilaya na kwenye maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ikiwemo ya ibada kama kanisani,misikitini pia gulioni na sokoni.

“Tunazo taarifa za kuwepo kwa ugonjwa wa polio pamoja na virusi vya polio kwenye maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo nchi mbalimbali zinazotuzunguka,na kwa sababu hiyo kama nchi kupitia Serikali tumeamua kuwakinga watoto wetu mapema kabla ugonjwa huu haujafika,”amesema Dkt.Magembe

Amesema chanjo hiyo ni salama na siyo mara ya kwanza kutolea kwani inatolewa kwa utaratibu wa kawaida kwenye vituo vyote,ambapo wa mama  ni mashahidi wakishajifungua  kabla hawajatoka hospitali mtoto anapewa matone ambayo  ni pamoja na chanjo hiyo ya polio.

Pia amesema,ugonjwa wa pilio unaweza kutoka kwa mtoto mmoja kwenda kwa mtoto mwingine ili   kuwakinga wanahitaji kuwachanja watoto wengi zaidi.

“Tukiwachanja wachache na wengi wakabaki hawajachanjwa wanaweza kuwa chanzo cha kuambukiza au mlipuko wa ugonjwa kwenye jamii,ndio maana tunasisitiza kuwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka 10 apate chanjo hiyo,”amesema Dkt.Magembe.

Kwa upande wake Daktari Florence Tinuga,kutoka ofisi ya Waziri Mkuu,amesema utoaji wa chanjo hiyo ni fursa muhimu kwa mikoa saba,ambayo kupitia uchunguzi waliona ipo kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa polio kwa watoto chini ya umri wa miaka 10.

Hivyo ametoa wito kwa watumishi wanaoshiriki katika zoezi hilo la utoaji chanjo katika mikoa yote saba, kuhakikisha wanawapata watoto wote waliolengwa katika kampeni hiyo huku akisisitiza kuwa ugonjwa wa polio hauna tiba bali ni kinga ambayo ni chanjo pekee,hivyo wazazi,walezi na wananchi wajitokeze kwa wingi kupeleka watoto wao.

“Mara nyingi siku za mwanzo hawajitokezi na badala yake hujitokeza siku ya mwisho ambayo watoto wanakuwa wengi,na muda unakuwa umeisha hivyo kufanya watoto wengi kubaki bila kupata kinga kupitia chanjo.Jambo ambalo siyo lengo letu,”amesema Dkt.Florence.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana,amesema Wilaya ya Magu pekee inalenga kuwafikia zaidi ya watoto 140,000 huku Mwanza ikiwa miongoni mwa mikoa yenye hatari kubwa ya maambukizi ya kirusi cha polio.