November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania wahimizwa kutembelea vivutio vya Utalii kuelekea kilele Cha siku ya wanawake Duniani

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imewataka Watanzania ikiwemo Wanawake kusherekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutembelea Vivutio vya Utalii vilivyopo nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Machi 7, 2024 na Afisa Utalii, Maria Nyamsekela akiwa katika Maonesho ya Wiki ya Wanawake yanayofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia leo kwenye Viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma .

Amesema Maadhimisho hayo yatumike kwa Watanzania ikiwemo Wanawake kwa kutembelea Vivutio vya Utaliii nchini ili waweze kujionea jinsi Tanzania ilivyobarikiwa kuwa na vivutio vya kila aina mathalan wanyamapori, fukwe, misitu, utamaduni na milima huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kuchangia uchumi wa nchi na kukuza Utalii wa ndani.

Ameongeza kuwa, Tanzania imejaliwa kuwa na maeneo mengi yenye Vivutio vya Utalii huku akitaja maeneo kama Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Hifadhi ya Nyuki Agondi, Pori la Akiba Mkungunero kuwa ni mfano wa maeneo machache mazuri ambayo Watanzania ikiwemo wanawake wanaweza kwenda kufanya Utalii wa ndani.

“Tanzania ni nchi iliyojaliwa vivutio mblalimbali, Tuna Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Hifadhi ya Nyuki Agondi, Pori la Akiba Mkungunero na maeneo mengi ya Malikale, Tunachotakiwa kufanya Siku hii ya Kilele cha Siku ya Wanawake ni kwenda kutembelea Vivutio vyetu kwa wingi na hapo tutakuwa tumechangia uchumi wa nchi yetu.’’ Amesema Nyamsekela

Sambamba na hayo, amewataka Watanzania wote kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii lilipo katika maonesho hayo ili waweze kupata maelezo ya namna ya kufika kwenye maeneo mbalimbali ya Vivutio hivyo vya Utalii

‘’ Nitoe rai kwa Watanzania wote ikiwemo wakazi wa Dodoma kutembelea Banda letu la Wizara ya Maliasili na Utalii ili waweze kujionea Vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo na pia waweze kupata maelezo ya namna gani ya kufika kwenye vivutio vyetu vya utalii hapa nchini’’

Naye, Juma Salim akitembelea Banda la Wizara katika maonesho hayo, ameipongeza Wizara kwa kuendelea kutumia njia mbalimbali ikiwemo Maonesho mbalimbali nchini kutangaza Utalii wa ndani.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila mwaka Machi 8 ambapo kwa mwaka huu Kifaita yatafanyika Jijini Dodoma katika Wilaya ya Chamwino yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘’ Wekeza kwa Wanawake kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi kwa Jamii’’