May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi wa Marekani akunwa na Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

BALOZI wa Marekani, Battle Harris, ameupongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo umekuwa wa wazi, imara na jasiri katika kusimamia misingi ya demokrasia na utawala bora.

Balozi huyo ametoa kauli hiyo juzi Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Nchimbi.

“Kama unavyojua uhusiano huu ni wa muda mrefu, ukaboreshwa zaidi na urafiki uliokuwapo kati ya (Mwalimu) Nyerere na (John) Kennedy. Lakini pia kulikuwa na ukaribu kati ya (Jakaya) Kikwete na (George) Bush na sasa tunaona ukaribu kati ya Rais Samia  na Makamu wa Rais (wa Marekani) Kamala Harris.

Napenda kukuhakikishia na ujue kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Marekani ni mkubwa na halisi,” alisema Balozi Battle.

Naye Balozi Nchimbi, amesema dhamira ya Mwenyekiti wa CCM,  Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora na hivyo haipaswi kutiliwa shaka hata kidogo.

Balozi Nchimbi amesema katika utekelezaji wa dhana ya utawala bora, chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeendelea kushuhudia kuwapo kwa uhuru wa mihimili mitatu ya dola, ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.

Amesema mihimili hiyo ya dola imeendelea kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi vizuri na hivyo kuaminiwa na wananchi.

Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa CCM chini ya Rais Samia, kitahakikisha dhamira hiyo pia inaendelezwa kwa vitendo kwa kuunga mkono uwapo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kwa maslahi ya nchi na taifa kwani umoja huo ni zaidi ya vyama vya siasa.

Katika mazungumzo yao, wamekubaliana nchi zote mbili kuangalia maeneo yanayoweza kuboreshwa kwa manufaa ya pande zote mbili hasa katika nyanja za biashara, uchumi na uwekezaji.

Vilevile, viongozi hao kwa pamoja wameelezea umuhimu wa kurahisishwa kwa upatikanaji viza.

“Ni wajibu wetu kuimarisha na kuuboresha uhusiano huu wa muda mrefu kama tulivyoupokea kutoka kwa waasisi na watangulizi wetu kama ulivyosema balozi.

Tuuboreshe kwa ajili ya manufaa ya wananchi wetu wa pande zote mbili,”anasema Balozi Nchimbi.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Michael Battle, walipokutana Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam, kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, Machi 5, 2024.