Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
TAKRIBANI Maofisa Maendeleo ya Jamii 1260,kutoka katika taasisi mbalimbali ikiwemo za umma hapa nchini, wanatarajia kukutana mkoani Mwanza ,ili kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo changamoto na mchango wao katika kufanya taifa linakuwa na maendeleo endelevu.
Akizungumza leo Juni 15,2026 na waandishi wa habari jijini Mwanza,Rais wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania(CODEPATA),Victor Kabuje,amesema chama hicho kinatarajia kufanya mkutano .Mkuu wa mwaka kwa siku tatu kuanzia Juni 17 hadi 19,2026 mkoani hapa.
Ambapo mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa Juni 17,2026 na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais(Maendeleo ya Vijana),Dkt.Joel Nanauka,huku muongoza mada Mkuu atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka.
Kabuje,amesema pia kupitia mkutano huo watatambulisha taaluma ya Maendeleo ya Jamii kwani imeonekana kuwepo kwa ombwe kwa wananchi kutoifahamu pamoja na kuishauri Serikali kuwatumia Maofisa hao katika utekekalezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Pia wanatarajia kuanzisha Dawati la Maofisa Maendeleo ya Jamii kwa kila Wizara ili kuhakikisha shughuli wanazozifanya zinawafikia wananchi.
“Katika mkutano huu tutazindua Bodi ya Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii,ambayo itasimamia chama na Mwenyekiti wake atakuwa Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda.Pia tutapokea taarifa ya mwaka ya chama na nini tunaenda kufanya kwa mwaka huu,”amesema Kabuje.
Hata hivyo amesema Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wana nafasi muhimu katika kutafsiri na kusimamia utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa manufaa ya wananchi wote.
Vilevile amesema chama hicho kitaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuhamasisha wananchi kuachana na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na ustawi wa jamii.
Kwa upande wake Katibu wa CODEPATA Sigilinda Mdemu,amesema mkutano huo utafanya tathmini ya kazi zinazofanywa na Maofisa Maendeleo ya Jamii katika maeneo mbalimbali.
Huku akisisitiza kuwa Maofisa Maendeleo ya Jamii wapo katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika taasisi za umma,binafsi na za dini na ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi.

More Stories
TASHICO,LMC waingia makubaliano usafirishaji majini
Wasomi wahimizwa kuelimisha jamii na kulinda Taswira
Tulia Trust yaanza ujenzi nyumba ya Andembwisye