Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Korea,
SESERIKALi ya anzania imewasilisha hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua kwa kushirikiana na UNESCO, Mashirika ya Ushauri ya IUCN na ICOMOS pamoja na wadau wengine wa kimataifa katika kuhakikisha Eneo la Hifadhi la Ngorongoro linaendelea kuhifadhi Hadhi yake ya Urithi wa Dunia huku likiimarisha ustawi wa wananchi.
Hatua hizo ziliwasilishwa katika semina maalum iliyoandaliwa na Tanzania pembezoni mwa Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia cha UNESCO kinachoendelea mjini Busan, Jamhuri ya Korea.
Semina hiyo ilihudhuriwa na mabalozi na wawakilishi wa nchi 36, viongozi wa kimila, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, taasisi zisizo za kiserikali, wataalamu wa uhifadhi pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya urithi wa dunia.

Akifungua semina hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Saidi Yakubu, alisema Tanzania inaamini kuwa uhifadhi endelevu wa maeneo ya urithi wa dunia unahitaji uwazi, mazungumzo ya kujenga na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi na jumuiya ya kimataifa.
Ameeleza pia kuwa Tanzania imeialika rasmi UNESCO pamoja na Mashirika ya Ushauri ya IUCN na ICOMOS kufanya Ziara ya Ufuatiliaji (Reactive Monitoring Mission) katika Eneo la Hifadhi la Ngorongoro.
Mbali na hotuba ya Balozi Yakubu, washiriki walisikiliza mada zilizowasilishwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO (NATCOM), Profesa Malebo, pamoja na Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambaye pia alikuwa mratibu wa semina hiyo. Mada hizo zilieleza historia ya Ngorongoro, thamani yake ya kipekee duniani, changamoto zinazoikabili na hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha uhifadhi unaenda sambamba na maendeleo ya wananchi.
Akichangia mjadala, Mkurugenzi wa Kituo cha Urithi wa Dunia cha UNESCO, Lazare Eloundou Assomo, aliipongeza Tanzania kwa ushirikiano wake wa karibu na UNESCO, IUCN, ICOMOS na jamii husika, akieleza kuwa mazingira hayo ya ushirikiano yamewezesha kufikiwa kwa makubaliano ya kutuma ujumbe wa wataalamu wa UNESCO katika siku za karibuni kwa ajili ya kufanya Ziara ya Ufuatiliaji katika Ngorongoro.
Naye Mwakilishi wa Kudumu wa Falme za Kiarabu (UAE) katika UNESCO, Balozi Ali Abdullah Al Ali, alisema semina hiyo imekuwa ya kufungua macho kwa washiriki kwa kuwa imefafanua historia ya makundi mbalimbali ya jamii yaliyohamia Ngorongoro kwa nyakati tofauti, asili ya mfumo wa matumizi mseto ya ardhi ulioanzishwa mwaka 1959 pamoja na changamoto zinazotokana na ongezeko la watu na mifugo. Alipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka ustawi wa wananchi kuwa kipaumbele katika kutekeleza wajibu wake chini ya Mkataba wa Urithi wa Dunia na kueleza kuwa Tanzania inaweka mfano mzuri unaostahili kuigwa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Armenia katika UNESCO, Balozi Aram Hakobyan, alisema semina hiyo imeongeza uelewa kuhusu historia ya Ngorongoro na utofauti wa jamii zinazoishi ndani na kuzunguka eneo hilo, ikiwemo Wamasai, Wadatoga, Wairaqw na Wahadzabe. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikisha makundi yote katika hatua za kuboresha ustawi wa jamii na kuimarisha uhifadhi wa eneo hilo.
Washiriki wengi waliipongeza Tanzania kwa kuandaa semina hiyo wakieleza kuwa imeongeza uelewa kuhusu hali halisi ya Ngorongoro na kupendekeza kuendelea kuwepo kwa programu za elimu na mawasiliano zitakazowezesha wadau wa kimataifa kupata taarifa sahihi kuhusu juhudi za uhifadhi zinazotekelezwa na Serikali.
Semina hiyo ilihitimishwa kwa mjadala wa wazi na kutazama filamu kuhusu Ngorongoro, huku Tanzania ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na UNESCO na wadau wote wa kimataifa katika kulinda Thamani ya Kipekee ya Kimataifa ya Eneo la Hifadhi la Ngorongoro kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.


More Stories
Wizara ya maliasili na utalii yawasilisha rasimu ya miaka mitano
HGWT yaahidi kutekeleza mkakati wa kutokomeza ukeketaji
Alizeti yawa zao kimbilio kwa wakulima Chunya