June 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasomi wahimizwa kuelimisha jamii na kulinda Taswira

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WASOMI wa vyuo vikuu nchini wamehimizwa kutumia elimu na utaalamu wao kuielimisha jamii pamoja na kushirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali katika kukuza amani, umoja na taswira ya Tanzania.

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa (MNEC), Ndele Mwaselela, alipokutana na Shirikisho la Wasomi wa Vyuo Vikuu kutoka wilaya saba za Mkoa wa Mbeya.

Amesema wasomi wana nafasi muhimu katika kutoa taarifa sahihi kwa jamii na kuchangia mijadala ya maendeleo, akieleza kuwa ushiriki wao unaweza kusaidia kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kulinda sifa ya nchi.

Mwaselela amesema uwekezaji katika elimu umeongeza idadi ya wasomi nchini, hivyo kuna umuhimu wa kutumia maarifa hayo katika kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi.

Pia amesema wasomi wanapaswa kuendana na mabadiliko ya dunia kwa kutumia fursa zinazojitokeza katika uchumi wa kidijitali, akieleza kuwa teknolojia imefungua njia mpya za ajira na ujasiriamali kwa vijana.

Akizungumzia maendeleo ya taifa, amesema amani na utulivu ni miongoni mwa nguzo muhimu zinazowezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kufanyika kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amesema mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri imeendelea kusaidia makundi mbalimbali kiuchumi, huku vikundi 564 vikifaidika na mpango huo na kuchangia upatikanaji wa ajira.

Naye Rhoda Juma amesema wananchi wanapaswa kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuunga mkono juhudi zinazolenga kuboresha ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.