May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanufaika TASAF waeleza mafanikio yao

Na Lubango Mleka, TimesMajira Online

KIPINDI cha pili cha TASAF awamu ya tatu ni kuanzia 2020 – 2023, ambapo kipindi hiki kinatekelezwa katika Mamlaka za Utekelezaji 187, ambazo ni halmashauri zote za Tanzania Bara, Unguja na Pemba.

Mpango huu unatekelezwa katika vijiji,mitaa na shehia zote nchini na walengwa wa mpango katika kipindi hiki ni kaya milioni moja na laki nne( milioni 1.4) zenye watu wanaokadiriwa kuwa takribani milioni 7.

Madhumuni ya kipindi cha pili ni kuongeza fursa za kujiongezea kipato na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa kaya za walengwa na kulinda maslahi ya watoto wao.

Malengo ya kipindi hiki cha pili yatafikiwa kwa kutekeleza shughuli mbalimbali kupitia sehemu kuu tatu ambazo ni uwasilishaji wa fedha ambao utaongeza kipato cha kaya na kuwekeza katika afya na elimu ya watoto, kuinua uchumi wa kaya kwa kujenga uwezo kwa kaya katika utunzaji rasilimali na kutengeneza njia mbadala na endelevu za ajira.

Pia kushiriki katika kazi za jamii na kupata kipato cha ziada kwa matumizi ya kaya kama chakula na kugharamia mahitaji mengine ya msingi na wakati huo wakiboresha miundombinu katika jamii na kupata ujuzi na stadi za maisha.

Mmoja wa wanufaika wa TASAF Mkazi wa kijiji cha Ganyawa, Kata ya Mbutu Wilaya ya Igunga mkoani Tabora Ruli Jimoku akitoka kwenye nyumba yake ya tembe aliyokuwa akiishi kabla hajafikiwa na TASAF.

Katika kuhakikisha jamii ya wanaigunga ambao ni wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo Jamii (TASAF) Halmashauri ya Wilaya ya Igunga imekuwa ikifuatilia na kuendelea kutoa elimu kwa wanufaika wa mpango huo kwa kuwatembelea na kukagua shughuli wanazozifanya za kuinua vipato na kiuchumi.

Baadhi ya wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Kijiji cha Ganyawa Kata ya Mbutu Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wameeleza jinsi walivyopata mafanikio kwa muda mfupi kupitia fedha wanazopewa na serikali kwa ajili ya kuwathamini wananchi wake katika suala zima la kutatua wimbi la umaskini hapa nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kijijini hapa baada ya kutembelewa na viongozi wa ngazi ya Wilaya akiwemo mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo, ambaye ni Ofisa Tarafa ya Manonga, Maritha Tevely aliyeambatana na Ofisa ufuatialiaji TASAF Wilaya ya Igunga Zahara Mbailwa.

Baadhi ya wanufaika hao akiwemo Ruli Miyanga wa kitongoji cha Mashariki (B) katika Kijiji cha Ganyawa,anaishukuru serikali kwa kuendeleza mpango huo wa kunusuru kaya maskini kwa kutoa kiasi cha fedha hizo ambazo zimewaondoa kutoka kwenye wimbi la umaskini wa kupindukia waliokuwa nao miaka mingi.

“Kabla sijafikiwa na TASAF nikuwa na maisha magumu sana, miongoni mwa shida  nilizopitia ni pamoja na kulala chini kwa kutandika naironi au nguo,changamoto nyingine ni kulala njaa mara kwa mara, kukosa mavazi na kuishi kwenye nyumba ya tembe ambapo usiku nilikua nakumbana na udongo uliokuwa ukimdondokea mwilini kutoka juu ya tembe langu,”amesema Miyanga.

Amesema kuwa, mwaka 2022 alibahatika kuingia kwenye mpango huo wa
TASAF ambapo awamu ya kwanza alipokea kiasi cha shilingi 48,000
na alipozipata fedha hizo aliamua kununua dagaa na nyanya na kuanza biashara ya kutembeza  kijijini hapo huku kiasi kingine cha fedha akinunua chakula na nguo za watoto wake.

Pia amesema kuwa biashara hiyo ilikuwa inamwingizia kipato kikubwa sana cha fedha na alipoona amepata fedha nyingi aliamua kununua mbuzi wawili wa kike na kuanza ufugaji ambapo hadi hivi sasa amefikisha mbuzi wanne, pia suala la chakula ameweza kudhibiti kwa kununua mahindi ya chakula ya kutosha.

Mmoja wa wanufaika wa TASAF Mkazi wa kijiji cha Ganyawa, kata ya Mbutu wilaya ya Igunga mkoani Tabora Ruli Jimoku katikati akiwa kwenye nyumba yake mpya baada ya kuingia katika mpango wa TASAF

Hata hivyo, Miyanga baada ya kuona kuwa amemudu baadhi ya changamoto alizokuwa nazo alitenga fedha zingine kwa ajili ya kununua mabati ambapo aliamua kutafuta mabati makuu kuu yaliyotumika ambayo amefanikiwa kujenga nyumba yenye chumba kimoja na sebule moja na hivi sasa anashughulikia kuweka milango na madirisha.

Aidha aliongeza kuwa, fedha hizo zimemsaidia kununua nguo za shule na za nyumbani kwa watoto wake watatu ambao ni Kondela Mahushi anayesoma darasa la nne shule ya msingi Ganyawa , Gelesoni Manuel darasa la kwanza shule ya  msingi Ganyawa na Geofrey Nyorobi ambaye bado hajaanza shule kutokana na umri mdogo.

Kwa upande wake Milembe Kashindye ambaye ni mnufaika wa TASAF amesema yeye anapokea shilingi 56,000 kila awamu, ambapo baada ya kupata fedha hizo mwaka 2022 aliamua kutengeneza kisanduku kwa jina maarufu ‘kibubu’ cha kuhifadhia fedha hizo huku zingine akinunua mbuzi ambapo hadi sasa ana mbuzi watano.

Milembe aliongeza kuwa  fedha hizo zimeweza kumsaidia kulima hekali nne za zao la pamba na hadi sasa amevuna kilo 350 na bado anaendelea kuvuna pamba hiyo na kufafanua kuwa anategemea kupata zaidi ya kilo 700  ambapo fedha hizo anategemea kununua  ng’ombe jike mmoja ambaye akizaa ng’ombe wengine atakuwa ameongeza kipato na kuwaachia wengine wanufaike na mpango huo wa TASAF.

Sanjari na mafanikio hayo, pia amefanikiwa kuvuna gunia mbili za  zao la choroko ambazo tayari ameuza kiasi cha shilingi 220,000 na fedha hizo baadhi zilimsaidia kuweka vibarua wa kupalilia shamba la pamba.

Ameongeza kusema ataendelea kuishukuru serikali katika maisha yake kwa kuwajali wananchi wake.

Huku Mtendaji wa kijiji cha Ganyawa Chelehani Jisinza amesema tangu mpango huo uanze katika kijiji chake Januari 16/2022 kiasi cha zaidi ya milioni 55 zimekwishatolewa kwa  kaya zilizopo 126 zinazonufaika na TASAF kijijini hapo.

Aidha Mtendaji huyo wa Kijiji amesema tangu kaya hizo zianze kupokea ruzuku hiyo wanufaika wengi wa kaya hizo wameanzisha miradi midogo midogo ya kilimo na ufugaji wa mifugo ikiwemo mbuzi, kuku, bata na kondoo ili kujikomboa  kimaisha.

Pia kaya zimewezesha wanafunzi kuhudhuria shule na kliniki kwa kuwa hupewa ruzuku kwa ajili ya mahitaji ya shule.

Ofisa ufuatiliaji wa TASAF Wilaya ya Igunga Zahara Mbailwa, amesema wanufaika wengi wa TASAF wameondokana na wimbi la umaskini kutokana na uelewa mkubwa wa kuzitumia fedha hizo katika miradi ya kilimo, ufugaji, ujenzi wa nyumba za kuishi huku akiahidi kuendelea kutoa elimu kwa walengwa.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Igunga Martha Tevely amewataka wazazi kushirikiana na walimu kuhakikisha watoto wote wanapata chakula shuleni ili kuwajengea mazingira mazuri kielimu, aidha ametoa wito kwa wazazi kuachana na vitendo vya anasa kwa kuwa vinaleta umasikini katika jamii.