Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wanawake wa Jeshi la Magereza kuendelea kujijengea uwezo, kuongeza elimu na ujuzi ili kupata nafasi mbalimbali za uongozi na kitaaluma katika Jeshi hilo.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kutumia fursa za kidijitali katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhandisi Mahundi ametoa kauli hiyo Septemba 7, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mtandao wa Wanawake Jeshi la Magereza Tanzania 2026, unaolenga kuwajengea uwezo wanawake, kukuza uongozi, kuimarisha usawa wa kijinsia na kuongeza ufanisi katika majukumu ya urekebishaji wa wafungwa.
Amesema uwezeshaji wa wanawake ni sehemu muhimu ya kujenga mtaji wa watu wenye uwezo, akiwataka wanawake wa Jeshi la Magereza kuwa mstari wa mbele katika mageuzi ya kijamii na kidijitali ya Jeshi hilo.
“Nawahimiza wanawake wa Jeshi la Magereza kujiamini, kuongeza elimu na ujuzi, na kujiandaa kwa ushindani wa haki katika nafasi za uongozi na kitaaluma. Katika dunia ya sasa, watumishi wanapaswa kuendelea kujifunza na kutumia teknolojia katika kuboresha huduma,” amesema Mhandisi Mahundi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Divisheni ya Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP Nicodemus Menyiansumba Tenga, amesema mafanikio ya wanawake waliopo katika nafasi mbalimbali kwenye Jeshi hilo ni mfano unaopaswa kuhamasisha wengine.
Akisoma taarifa ya Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza Tanzania (TPSWNet), Kamishna wa Huduma za Urekebishaji Jeshi la Magereza, CP Amina Jumanne Kavirondo, amesema mtandao huo umeendelea kuwa chombo muhimu katika kuwajengea wanawake uwezo, kukuza usawa wa kijinsia katika majukumu ya kazi, kuweka mazingira rafiki ya kazi kwa wanawake na kuhakikisha uwakilishi wao ndani na nje ya Jeshi pale inapowezekana.
Aidha, amesema kuongezeka kwa ufanisi wa kazi miongoni mwa watumishi wanawake kunaonekana kupitia shughuli za urekebishaji wa wafungwa zinazofanywa magerezani, ikiwemo kuwapatia wafungwa ujuzi pamoja na kushiriki katika masuala ya ulinzi na usalama.
Amesema mkutano huo pia unalenga kuwajengea wanawake uwezo katika uongozi, kujitambua na kufanya maamuzi, kubadilishana ujuzi wa kitaifa, kikanda na kimataifa kuhusu jukumu la urekebishaji wa wafungwa, pamoja na kujadili malezi, maendeleo ya awali ya mtoto na wajibu wa kijamii.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mtandao wa Wanawake Jeshi la Magereza Tanzania 2026 unafanyika jijini Dodoma kuanzia Septemba 7 hadi 9, 2026, ukiwakutanisha wanawake wa Jeshi la Magereza pamoja na wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili masuala ya uongozi, uwezeshaji wa kiuchumi, maadili, afya, matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na urekebishaji wa wafungwa.
Mkutano huo umebeba kaulimbiu: “Wanawake Mahiri, Jeshi la Magereza la Kisasa, na Taifa lenye Ustawi kuelekea Dira 2050.”

More Stories
Aweso amrejesha Mha.Msenyele kuongoza MWAUWASA
GBT yawataka wachezaji kucheza kwa kiasi
Serikali yaongeza kasi kutatua kero ya maji Mwanza