September 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaongeza kasi kutatua kero ya maji Mwanza

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza

SERIKALI  kupitia Waziri wa Maji Jumaa Aweso,imesema  hakuna sababu ya Jiji la Mwanza kuwa na  changamoto ya mgao wa maji,hivyo imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuongeza kasi ya kukamilisha ujenzi wa matenki matano yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita milioni 31 za maji pamoja na kuboresha vyanzo vya maji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka katika jiji hilo.

Aweso amesema hayo Septemba 7,2026 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Mfumo wa Usambazaji Maji Mwanza Kusini unahisisha ujenzi wa matenki matano na kutoa cha kusukuma maji,ambapo amesema,Serikali inatambua ongezeko la watu na mahitaji makubwa ya maji katika Jiji la Mwanza, hivyo imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha uzalishaji wa maji unaongezeka na maji hayo yanafika kwa wananchi.

Miongoni mwa hatua hizo ni ujenzi wa chanzo cha maji Butimba, kinachoongeza zaidi ya lita milioni 48 za maji.

Aweso amesema,uzalishaji wa maji pekee hautoshi endapo hakuna mfumo madhubuti wa kuyafikisha kwa wananchi, ndiyo maana Serikali imewekeza katika ujenzi wa matenki matano katika maeneo ya Buhongwa, Fumagila, Kisesa, Nyamazobe na Usagara, na sehemu kubwa ya majengo ya matenki imekamilika huku kilichobaki nia masuala la kiufundi.

Ili  wananchi waanze kunufaika na huduma ya maji mapema,Aweso amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kuitisha kikao cha haraka kati ya mkandarasi,timu ya ufundi ya wizara  hiyo na mshauri wa mradi,kwa ajili ya kuangalia namna ya kupunguza muda wa utekelezaji, kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha vifaa vyote vinavyohitajika vinapatikana katika eneo la mradi.

Sanjari na hayo Aweso amesema,Serikali inaendelea na mpango wa kuongeza uzalishaji katika chanzo cha Capripoint, ambacho kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 90 kwa siku. Mradi huo unaotekelezwa na SUMA JKT kwa gharama ya zaidi ya sh.bilioni 22,ambao utaongeza uzalishaji hadi lita milioni 144 kwa siku.

Ambapo ongezeko hilo litasaidia kukabiliana na upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza, ikiwemo Buswelu,Kahama,Kiseke na Kishiri huku akisisitiza kuwa Serikali haitaki maji yanayozalishwa yabaki kwenye vyanzo bali yafike kwa wananchi.

Katika hatua nyingine amesema,Serikali ilifanya mabadiliko ya kiutendaji katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) baada ya kubaini changamoto mbalimbali, ikiwemo uzembe wa baadhi ya watumishi na mapungufu katika ukusanyaji wa mapato.

Hatua hizo zimeanza kuleta matokeo, ambapo zaidi ya wananchi 2,000 waliokuwa wamelipia kuunganishiwa maji lakini hawakupata huduma hiyo sasa wameunganishiwa, huku zaidi ya sh.milioni 700 ambazo awali yazekena zilikuwa zinaenda kwenye mifuko ya watu na  hazionekani  kwenye  taasisi,sasa  zimepatikana na kuwezesha watumishi kupata mishahara na shughuli nyingine kuendelea.

Kwa upande wake, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele amesema,mahitaji ya maji jijini  Mwanza ni makubwa kuliko uwezo wa vyanzo vilivyopo, hali iliyosababisha Serikali kuwekeza katika miradi mipya ya uzalishaji na usambazaji ya chanzo cha maji Butimba.

Mha.Msenyele amesema,matenki matano yanayojengwa kupitia mradi  wa mfumo wa usambazaji maji Mwanza Kusini ni Buhongwa na Fumagila kila moja lina uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10, Kisesa lita milioni tano,Nyamazobe lita milioni tano na Usagara lita milioni moja pamoja na kituo cha kusukuma maji cha Sahwa huku mradi mzima ukigharimu takribani sh.bilioni 46.

Amesema,Serikali pia inaendelea na awamu ya pili ya upanuzi wa chanzo cha maji  Butimba, ambapo uzalishaji utaongezeka kutoka lita milioni 48 hadi lita milioni 70 kwa siku, sambamba na kuboresha chanzo cha maji  Capripoint kutoka lita milioni 90 hadi  lita milioni 144 kwa siku.

Naye Mbunge wa Jimbo la  Ilemela, Kafiti Kafiti amesema, mradi huo wa matenki matano  umefikia asilimia 80 na unaelekea kukamilika, huku akieleza kuwa yeye pamoja na Mbunge wa Nyamagana wanaendelea kushirikiana katika kuhakikisha changamoto ya maji katika majimbo hayo inamalizika.