Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza
WAZIRI wa Maji,Jumaa Aweso, amefanya mabadiliko ya uongozi katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA),ambapo amemteua Mhandisi Leonard Msenyele kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka huku aliyekuwa Mkurugenzi wa mamlaka Mhandisi Mashaka Sitta, akihamishiwa Wizara ya Maji kuwa Msimamizi wa Miradi ya Maji hapa nchini.
Hata hivyo Mha.Sitta alikabidhiwa kijiti cha kuongoza MWAUWASA na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka hiyo Nely Msuya,ikiwa imepita miezi kadhaa mara baada ya Aweso, kuvunja menejimenti ya MWAUWASA, akisema hakuridhishwa na kiwango cha utoaji huduma ya maji jijini Mwanza na kubaini changamoto za kiutendaji.
Huku Mha.Msenyele akiwa si mgeni katika nafasi hiyo kwenye mamlaka hiyo kwani mwaka 2019 aliteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA na baadae Mkurugenzi kamili ambapo safari yake ilihitimishwa mwaka 2023 baada ya Aweso kumtengua katika nafasi hiyo.
Hata hivyo leo Septemba 7,2026,wakati Waziri huyo alipoamua kumrejesha katika nafasi hiyo baada ya watumishi na wafanyakazi wa mamlaka hiyo kumpendekeza Mha.Msenyele alikuwa anatumika katika nafasi ya Kaimu Mkurugenzi wa Usambazaji na Usafi wa Mazingira MWAUWASA.
Akizungumza na menejimenti na watumishi wa MWAUWASA jijini Mwanza Leo,Aweso amesema,Mha.Msenyele ana jukumu la kurejesha heshima ya mamlaka hiyo, akimtaka kuwa kiongozi anayefuatilia changamoto za wananchi badala ya kukaa ofisini.
Huku akimsisitiza kuwatumia watumishi wa MWAUWASA kama nguzo muhimu katika kurejesha ufanisi wa taasisi hiyo, akisisitiza kuwa watumishi ndio wanaoweza kuinua au kuangusha taasisi.
“Watu watakaokuangusha ama kukuinua ni watumishi wako.Wajali na wasikilize, wajione wao ni sehemu ya taasisi. Nataka ukarejeshe heshima ya MWAUWASA,hatutaki Mkurugenzi wa ofisi, bali anayehangaika na changamoto za wananchi,”amesema Aweso.
Pia amemtaka Mha.Msenyele kuonesha mabadiliko ndani ya miezi mitatu, hasa katika kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza.
Amesema moja ya changamoto zinazopaswa kushughulikiwa ni upotevu wa maji unaofikia asilimia 42, akitaka MWAUWASA kubaini yanapopotelea na kuchukua hatua za haraka kuhakikisha maji yanawafikia wananchi.
“Mnasema asilimia 42 ya maji yanapotea,mnashindwa kujiuliza maji haya yako wapi? Semeni asilimia 42 ya fedha zinapotea, je, mfanyeje kuboresha?.Huu ni wizi wa kibiashara; inakuwaje mnazalisha maji yanachepushwa? Twende tukaitafute hiyo asilimia 42 ili wananchi wapate maji,” amesisitiza Aweso.
Akizungumza kuhusu uteuzi wa Mha. Sitta,Aweso amesema,amempa dhamana hiyo kutokana na uwezo aliouonesha katika utekelezaji wa miradi ya maji,huku akimtaka kutumia nafasi hiyo kusimamia miradi mikubwa ya wizara hiyo pamoja kuhakikisha mradi wa maji wa Capripoint jijini Mwanza unakamilika ambao utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 90 hadi lita milioni 144 kwa siku.
“Katika kipindi kifupi Mha.Sitta aliweza kukusanya sh.milioni 700 na kuwaunganisha wateja 2,000 katika huduma ya maji ya WAUWASA.Nakupa malengo, kazi ya kwanza nzuri lakini Mwanza usiitupe,”amesema.Aweso.
Aidha, Aweso amesema, Serikali imewaamini watendaji hao kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama, hivyo kushindwa kutekeleza wajibu huo ni kutomtendea haki Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake.
Hata hivyo amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuacha uzembe,kwani mafanikio ya taasisi yanategemea uwajibikaji wa kila mmoja.
“Kufanya kazi kuna faida,maneno matupu yanaleta hasara,Kwa heshima ya mliyoyafanya,moyo wangu una shukrani kwani ukimaliza kazi unavikwa taji,”amesema Aweso.

More Stories
TANESCO yatunukiwa Tuzo kutambua mchango wake
wanawake magereza wahimizwa kujenga uwezo , kutumia fursa kidijitali
GBT yawataka wachezaji kucheza kwa kiasi