May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaume waonywa maambukizi VVU

Na Israel Mwaisaka,TimesMajira Online,Sumbawanga

MKUU wa Wilaya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda amewataka wanaume kuacha kuwafanya wake zao kama vipimo vya Ukimwi na kuwa jukumu hilo ni la kila mmoja.

Ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo kiwilaya yalifanyika katika Kata ya Mtenga ambapo amedai kuwa wanaume wengi wamekuwa waoga kwenda kupima afya na wake zao wanapokuwa wajawazito utegemea kuwa majibu ya mke wake naye yanamhusu.

Amesema kuwa, sasa umefika wakati kwa kila mmoja kwenda kupima na kuijua afya yake na kuacha kutegemea majibu ya wake zao kwani kuna wakati mme anaweza kuwa na maambukizi, lakini mke asiwe nayo na ndiyo maana wanasisitiza kila mmoja kupima na kuitambua afya yake

“Ipo haja kwa kila mmoja kuitambua afya yake kwa kwenda kupima kitendo cha kuwategemea wanawake katika vipimo si sahihi,hivyo umefika wakati kwa kila mmoja kuitambua afya yake kwani kuna wakati inawezekana vipimo vikatofautiana kati ya mume na mke, hivyo jukumu la kupima afya ni kila mmoja,”alisema.

Pia amedai kuwa, katika tafiti mbalimbali za awali juu ya upimaji inaonyesha kuwa upimaji katika ngazi ya familia ni wa chini sana na kuwa ipo haja kwa wataalamu wa afya kuendelea kuihamasisha jamii kujua umuhimu wa kupima afya zao hasa katika mgazi ya familia.

Awali mratibu wa Ukimwi wa mkoa, Joseph Budeba amesema kuwa lengo kuu la siku ya Ukimwi duniani ni kukumbushana tu kwa jamii juu ya kukabiliana na Virusi Vya Ukimwi ikiwa ni pamoja na wale waliohathirika na ugonjwa huo kukwepa kupata maambukizi mapya.

Amesema kuwa ,wanaiadhimisha siku hiyo ya Ukimwi duniani huku kukiwa na mafanikio makubwa katika eneo la upokeaji wa matokeo kwa wanaopima ukilinganisha na siku za nyuma na kuwa katika siku hii ya Ukimwi ikawe ni ya kuleta mapinduzi makubwa juu ya kukabiliana na maambukizi mapya ya Ukimwi ikiwa ni pamoja na kuyafikia malengo ya kuutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani mwaka huu yamebeba ujumbe usemao “Mshikamano wa kitaifa,Tuwajibike kwa pamoja”