May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sensa Kilimo, Mifugo, Uvuvi yaokoa bilioni 5

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

SENSA ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka 2019/2020 iliyotumia miezi miwili kuanzia Agosti 5, 2020 hadi Oktoba 2, imeokoa zaidi ya bilioni 5 kwani miaka ya nyuma ilikuwa ikitumia miaka mitatu huku gharama zilizokuwa zikitumika ni bilioni 10 na sasa kiasi kilichotumika kukamilisha sensa hiyo ni bilioni 5.

Matokeo ya sensa hiyo yameonesha kuwa, Kaya milioni 7.8 sawa na asimilia 65.3 ya Kaya zote nchini, zinajihusisha na shughuli za kilimo ambapo kati ya Kaya hizo, milioni 7.7 zinatoka Tanzania Bara huku Kaya 180,219 zikitokea Visiwani Zanzibar.

Takriban asilimia 65 ya Kaya hizo, zinajihusisha na shughuli za kilimo cha mazao tu, wakati asilimia 33 zikijihusisha na shughuli za Kilimo cha mazao na Mifugo, wakati asilimia 2 zikijihusisha na shughuli za ufugaji tu.

Hayo yameelezwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Albina Chuwa wakati wa mkutano wa kutoa taarifa kuhusu matokeo muhimu ya sensa ya Kilimo, Mifugo na uvuvi ya mwaka wa Kilimo 2019/20 uliofanyika Mkoani Mwanza ambapo kazi ya kukusanya taarifa za sensa hiyo kwa mwaka wa 2019/2020 ilitumia takribani miezi miwili kuanzia Agosti 5, 2020 hadi Oktoba 2 tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wanatumia miaka mitatu na kuokoa zaidi ya bilioni tano kwani awali walikuwa wanatumia bilioni 10 ila sasa wametumia bilioni 5.

Dkt.Albina amesema, hivi karibuni Tanzania ilifanya sensa ya tano ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/2020 lengo kuu likiwa ni kutoa takwimu sahihi wakati wa Kilimo, Mifugo na Ufugaji wa Samaki, ambazo zitakuwa msingi thabiti wa kupanga, kufuatilia na kutathimini mipango ya kilimo pamoja na kutayarisha sera na pia kufanya maamuzi sahihi.

“Malengo mahususi ya sensa yalikuwa ni pamoja na kutoa taarifa za kina katika uzalishaji wa mazao na mazao ya Mifugo, idadi ya mifugo, matumizi ya pembejeo, usindikaji wa mazao, uhifadhi na masoko, upatikanaji wa huduma za ugani kwa mazao na mifugo, ufugaji wa Samaki na Nyuki na baadhi ya viashiria vya umaskini ambapo taarifa za sensa hii zilizokusanywa zilihusisha, wakulima wa mashamba madogo na wakulima wa mashamba makubwa yapatao 1,198,” amesema Dkt.Albina.

Matokeo hayo yameonesha kuwa, Kaya milioni 7.8 sawa na asimilia 65.3 ya Kaya zote nchini, zinajihusisha na shughuli za Kilimo, kati ya hizo kaya milioni 7.7 kutoka Tanzania Bara na 180,219 ni kutoka Zanzibar huku asilimia 65 ya Kaya hizo, zikijihusisha na shughuli za kilimo cha mazao tu, wakati asilimia 33 zinajihusisha na shughuli za kilimo cha mazao na mifugo na asilimia 2 zinajihusisha na shughuli za ufugaji tu.

Pia amesema, matokeo ya sensa yanaonesha kuwa, tani milioni 9.1 za mazao makuu ya chakula kwa upande wa nafaka ikiwemo Mahindi, Mpunga na Mtama zilizalishwa ambapo Mahindi yalikuwa tani milioni 5.7 sawa na asilimia 62.5 ya nafaka, ikifuatiwa na Mpunga tani milioni 2.9 sawa na asilimia 32.1, Mtama tani 488,724 sawa na asilimia 5.4.

Sensa ya kilimo, mifugo na uvuvi ya mwaka 2007/08 ilionesha kuwa uzalishaji wa mahindi ulikuwa tani milioni 5.4, mpunga tani 1.4 na mtama tani 552,354 hivyo ni sawa na ongezeko la Mahindi kwa asilimia 4.1, Mpunga zaidi ya asilimia 100 na Mtama umepungua kwa asilimia 11.5 ambapo lengo ni kuendeleza uzalishaji.

Hata hivyo amesema, katika kipindi hicho tani milioni 1.6 za mazao makuu ya jamii ya mizizi yaani Muhogo, Viazi vitamu na Viazi mviringo zilizalishwa huku tani 599,461 za mbegu za mafuta kama Alizeti, Chikichi na Ufuta zilizalishwa ambapo kwa upande wa mazao makuu ya biashara, Kahawa iliyozalishwa ilikuwa tani 92,396, Chai tani 40,611, Pamba tani 445,972 na Karafuu tani 3,378.

Matokeo ya sensa yanaonesha kuwa hekta milioni 13.5 zililimwa mazao mbalimbali, kati ya hizo, asilimia 76.7 zilitumia mbegu za asili, asilimia 20.8 zilitumia mbegu bora, na asilimia 2.5 zilitumia mbegu za aina zote mbili huku katika mwaka wa kilimo 2019/20, hekta milioni 2.8 zilitumia mbolea na kati ya hekta hizo, asilimia 60.7 zilitumia mbolea za asili na asilimia 39.3 zilitumia mbolea za viwandani.

Dkt. Albina amesema, matokeo ya sensa yanaonesha kuwa Kaya za wakulima wadogo ziliweza kusindika mazao yao, ili kuongezea thamani kwa ajili ya soko ambapo mazao yaliyosindikwa kwa wingi na Kaya hizo kulinganisha na mazao mengine ni Mahindi tani 706,464, Mpunga tani 193,462 na Alizeti tani 113,289.

Vile vile amesema, kwa upande wa mifugo sensa hiyo ilihusisha aina mbalimbali za mifugo inayofugwa nchini ambapo aina kuu za mifugo zilizoainishwa katika taarifa hiyo ni pamoja na Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo, Nguruwe na Kuku ambapo matokeo ya sensa hiyo yanaonesha kulikuwa na makadirio ya Ng’ombe milioni 33.9, kati ya idadi hiyo wakulima wadogo walikuwa na Ng’ombe milioni 33.8 na mashamba makubwa yalikuwa na Ng’ombe 143,183.

Kutokana na takwimu hizo, Tanzania imeendelea kuwa nchi ya pili Barani Afrika kwa kuwa na makadirio ya Ng’ombe 33,943,183 wakati nchi ya Ethiopia ikiongoza kwa kuwa na Ng’ombe milioni 60.39 na mifugo mingine wakulima wadogo walikuwa na Mbuzi milioni 24.5 na mashamba makubwa yalikuwa na Mbuzi 33,347.

Aidha, wakulima wadogo walikuwa na Kondoo milioni 8.5 na mashamba makubwa yalikuwa na Kondoo 24,236 vilevile, wakulima wadogo walikuwa na Nguruwe milioni 3.2 na mshamba makubwa yalikuwa na Nguruwe 5,153. idadi ya Kuku ilikuwa milioni 87.7, kati ya idadi hiyo wakulima wadogo walikuwa na Kuku milioni 75.1 na mashamba makubwa yalikuwa na Kuku milioni 12.6.

Uzalishaji wa maziwa matokeo ya sensa yameonesha pia katika mwaka wa kilimo 2019/20, lita bilioni 3.1 za maziwa ya Ng’ombe na lita milioni 53.1 za maziwa ya Mbuzi zilizalishwa katika kaya za wakulima wadogo.

Kwa upande wa udhibiti wa wadudu wanaoeneza magonjwa ya mifugo, matokeo ya sensa yanaonesha kuwa, njia zilizotumika kudhibiti Kupe ni pamoja na dawa za kunyunyiza, dawa za kuogesha kwenye majosho na dawa za kupaka huku ufugaji wa Samaki
unaonesha kuwa, Kaya 30,261 zilijishughulisha na ufugaji wa Samaki wa aina mbalimbali kati ya hizo Kaya 21,704 sawa na asilimia 71.7 zilijishughulisha na ufugaji wa Samaki aina ya Sato na kuzalisha tani 10,690.

Mratibu Kanda ya Zanzibar wa zoezi la sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwalimu Juma Mohammed, amesema kwa upande wa Zanzibar utafiti kama huo uliofanyika 2007/8 Kaya takribani 132.000 zilikuwa zinajishughulisha na kilimo wakati ya mwaka 2019/20 ni Kaya 180,219 hii ni ongezeko la zaidi ya asilimia 57.

Mohammed, amesema idadi ya mwaka 2007/8 utafiti ulionesha Ng’ombe takribani 155,624 ila utafiti wa sasa wa mwaka 2019/20 inaonesha wanang’ombe karibu 270,457 , hilo ni ongezeko la takribani asilimia 73.9, Mbuzi mwaka 2007/8, 68,972 lakini utafiti wa mwaka 2019/20 unaonesha kuna Mbuzi takribani 110,410 ongezeko la asilimia 61.7 na upande wa Kondoo kunaonekana kuna maendeleo mazuri ambapo imeongezeka.

Taarifa hii ni sehemu ya matokeo ya awali ya takwimu za msingi zilizokusanywa katika Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2019/20. Taarifa za kina zitapatikana katika ripoti kubwa, ambayo inaandaliwa na itatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2021, imetekelezwa kwa pamoja kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar (OCGS), kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo zikiwemo, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Waziri Mkuu; Wizara ya Kilimo; Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Wizara ya Viwanda na Biashara; na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ya Zanzibar.