December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaowahifadhi wahamiaji haramu Shinyanga kukiona

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga

WAKAZI wa Mkoa wa Shinyanga wameombwa kuunga mkono Opresheni zinazoendeshwa na Idara ya Uhamiaji mkoani humo kwa kuwafichua wahamiaji haramu wanaoingia katika mkoa huo kwa kutumia njia za panya ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kamishina Jenerali wa Uhamiaji nchini CGI Dkt. Anna Makakala.

Ombi hilo limetolewa na Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Shinyanga,Rashidi Magetta wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea mikakati inayoendelea ya Opresheni dhidi ya wahamiaji haramu katika maeneo yote ya mkoa wa Shinyanga.

Magetta amesema Opresheni ya kuwasaka na kuwakamata wahamiaji haramu ni endelevu mkoani Shinyanga na kwamba ili iwe na mafanikio ni lazima pawepo na mchango wa raia wema wanaotoa taarifa kila wanapowabaini wahamiaji haramu hao.

Amesema kila Mtanzania mwenye mapenzi na nchi yake anapaswa kutoa ushirikiano kwa maofisa wa uhamiaji walioko karibu katika kila kata kwa kutoa taarifa za mtu au kundi la watu ambalo watalitilia mashaka ili waweze kukamatwa na kuhojiwa kufahamu ni raia wa nchi gani.

“Ndugu zangu waandishi wa habari,tusaidieni kuwaelimisha wananchi wetu juu ya madhara yanayoweza kusababishwa na wahamiaji haramu wanaoingia hapa nchini kwa kutumia njia za panya, watu hawa ni hatari kwa mstakabali wa Taifa letu.

“Na waelewe kwamba mwananchi yeyote anayempokea na kumhifadhi raia wa kigeni aliyeingia hapa nchini kinyume cha sheria za uhamiaji anakuwa amevunja sheria za nchi na zile za uhamiaji na hivyo akitiwa hatiani anaweza kupata adhabu ya kifungo au kulipa faini si chini ya shilingi milioni 20,” ameeleza Magetta.

Ameendelea kueleza ulinzi wa nchi ni dhamana ya kila mwananchi mahali popote alipo, hivyo mtanzania ye yote mwenye mapenzi ya nchi yake hapaswi kuwa miongoni mwa watu wanaohatarisha usalama wa nchi kwa kuwapokea na kuwahifadhi au kuwaajiri raia wa kigeni wanaoingia nchini kinyume cha sheria za uhamiaji.

Baadhi ya kundi la wahamiaji haramu wapatao 45 kutoka nchini Ethiopia ambao walikamatwa mwishoni mwa mwaka uliopita wakiwa wamefichwa na mmoja wa wananchi katika kijiji cha Mipa wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga (Picha na Suleiman Abeid)

Amesema wahamiaji haramu wanaoingia nchini kwa njia za panya wana madhara mengi ikiwemo suala la kuambukiza magonjwa hatari ikiwemo Ebola au hivi sasa kutokana na uwepo wa ugonjwa wa Uviko 19 kwa vile hakuna sehemu yoyote wanayokaguliwa afya zao pale wanapoingia hapa nchini.

“Mbali ya kutuletea magonjwa hatari, lakini pia baadhi yao huja kwa ajili ya kutaka kupandikiza chuki miongoni mwa raia hali inayoweza kusababisha kutokea machafuko kama inavyotokea katika baadhi ya nchi jirani, na wengine hujihusisha na vitendo vya unyang’anyi wa kutumia silaha kwa lengo la kupata mali.

“Idara yetu haitalegeza opresheni hizi zinazoendelea kwa ajili ya kupambana na wahamiaji haramu mkoani kwetu, maana iwapo tutalegeza itakuwa ni kusaliti sheria na maelekezo ya Serikali na pia viapo vya kazi zetu, sasa ili tufanikishe kazi hii, lazima wananchi wetu watuunge mkono,” ameeleza.

Magetta amewaonya mawakala wanaofanya kazi ya kuwapokea wahamiaji haramu huku akitaja mbinu wanazotumia wahamiaji hao kuingia nchini kwamba baadhi yao huvizia siku za magulio na minada katika maeneo ya mipakani na hivyo huingia kama watu wanaotafuta mahitaji yao na baada ya hapo hawarudi makwao.

Baadhi ya wahamiaji haramu kutoka nchini Burundi waliokamatwa wilayani Kahama wakifanya kazi za majumbani ikiwemo uuzaji maandazi na chai na wengine uchungaji wa mifugo ambao wote walirejeshwa nchini kwao kwa amri ya Mahakama.

Amefafanua kuwa katika minada hiyo kuna watanzania ambao ni mawakala wa kuwapokea na kuwasafirisha kwa njia za vificho katika maeneo mbalimbali nchini wakitumia magari madogo (Noah) zinazokwenda vijijini wakikwepa mkono wa sheria ambako huwatafutia kazi za kufanya ikiwemo kilimo, uchungaji wa mifugo na uchimbaji madini.

Magetta ametaja mafanikio ya opresheni zinazoendelea ambapo kati ya mwezi Februari, 2021 hadi Julai 31, mwaka huu walifanikiwa kukamata wahamiaji haramu wapatao 330 na baada ya kufanyiwa mahojiano na mchujo 143 miongoni mwao walifikishwa mahakamani na kuamriwa kuondoshwa nchini ambapo walirejeshwa makwao kupitia mipaka ya Kabanga na Murusagamba.

“Wahamiaji haramu 124 waliondoshwa nchini moja kwa moja kutokana na umri wao kuwa chini ya miaka 18, wengine 63 walilipishwa faini mbalimbali kuhalalisha ukaazi wao hapa nchini wakitakiwa kuzingatia sheria za nchi, na hawa walikuwa ni raia kutoka nchi za China na Zimbabwe,” alieleza Magetta.

Katika hatua nyingine Magetta ametoa wito kwa watanzania wenye nia ya kusafiri kwenda nje ya nchi wazingatie sheria kwa kuhakikisha wanafika katika Ofisi za Uhamiaji kupatiwa Hati halali za kusafiria ili kuepuka na wao kukamatwa katika nchi wanazokwenda.

“Niwaombe Watanzania wanaosafiri kwenda nje ya nchi yetu wajiepushe na maofisa uhamiaji vishoka wa mitaani, wafike katika ofisi zetu wakiwa na nyaraka zote muhimu ili waweze kupatiwa hati halali za kusafiria, waje tuwahudumie, lakini pia watupatie taarifa za wahamiaji haramu wanaowafahamu,” ameeleza Magetta.