March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yadhamiria kutimiza ndoto za wanafunzi

Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikari inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikiisha sekta ya elimu inapata muelekeo mpana na kutengeneza fursa kwa watoto wa kitanzania ili kutimiza ndoto zao za kusoma katika ngazi zote mpaka vyuo vikuu.

Ili kufanikisha hilo, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu kwa shule za msingi, Sekondari pamoja na kuongeza idadi ya vyuo vikuu nchini lengo likiwa ni kuwaandaa watoto kutimiza ndoto zao.

Waziri Mkuu amesema hayo leo alipokuwa katika muendelezo wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo Mkoani Tabora, ambapo pia ametembelea Shule ya sekondari ya wavulana ya Tabora na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora ambako pia amefurahishwa na matokeo ya ufaulu wa shule hizo kimkoa na kitaifa sambamba na maboresho ya miundombinu yaliyofanywa katika shule hizo kongwe.

“Mheshimiwa Rais kaleta fedha nyingi sana za sekta ya elimu, kaleta bilioni 1, akaleta tena milioni 500 na fedha nyingine bilioni 7 ambazo naamini zimeshafika na zitajenga madarasa 590 ikiwa ni maandalizi ya kuwapokea watoto wa kidato cha kwanza, hii bilioni 7 ni sehemu ya bilioni 29 ambazo zimesambazwa kwa ajili ya sekta ya afya na elimu makusanyo ambayo yametokana na miamala,”.

Pia hivi karibuni Rais Samia, ametoa kibali cha kuajiri walimu wa masomo ya sayansi ili kukabiliana uhaba wa walimu katika masomo ya sayansi ili kuweka uwiano sawa wa ufundishaji baina ya walimu na wanafunzi.

 “Tumefurahi sana kuona kuna Watanzania wenzetu wanajitolea tunajua wanafanya kazi, napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inalitazama suala hili kwa umakini mkubwa na ninaiagiza TAMISEMI kuhakikisha walimu hawa wapewe kipaumbele katika ajira, wameonesha uzalendo wa hali ya juu,”.

 Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora, Waziri Majaliwa amesema, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha shule zote kongwe zinakarabatiwa na kuzirudisha katika ubora na ili kuwa na mazingira rafiki ya ujifunzaji na ufundishaji.

Pia Waziri Mkuu ameliomba Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tabora kuweka utaratibu na kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika shule hizo.