May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayojihusisha na uwekezaji katika sekta ya kilimo JATU PLC,Peter Gasaya akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Dar es Salaam.

Wananchi washauriwa kuwekeza sekta ya kilimo

Na Penina Malundo,Timesmajira,Online
WANANCHI  wameshauriwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo  ili kilimo chao kiweze kuwa na tija na manufaa kwa kila kulima ambapo  watakuwa na uhakika wa uzalishaji na soko. 
Wito huo umetolewa  juzi mkoani Dar es Salaam  na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayojihusisha na uwekezaji katika sekta ya kilimo  JATU PLC, Peter Gasaya, katika hafla ya uzinduzi wa uuzaji wa awali wa hisa za Kampuni hiyo kwa wananchi.
Amesema shabaha yao ni kuhakikisha sekta ya kilimo inafanyika kwa tija na kuwanufaisha wakulima hivyo, wameingia katika soko la hisa ambapo  kwa sh. 5,000 mwananchi atamiliki hisa 10 na kumuwezesha kulima na JATU PLC.
Gasaya amesema faida ya hisa hizo sio kulima na kampuni hiyo pekee, bali mwanahisa pia atapata faida kutokana na uwekezaji wake. 
“Hisa moja ya JATU PLC inauzwa sh. 500 hivyo kiwango cha awali ni hisa 10 ambazo mwananchi atazinunua kwa sh. 5,000, tumeweka kiasi hiki tukiamini ni rafiki kwa Watanzania na Kampeni hii tumeiita ‘buku tano inatosha’,” alisema. 
Gasaya amesema uwekezaji huo unalenga kupatikana kwa zaidi ya sh. bilioni saba, ili kufanikisha utekelezwaji wa mradi wa Kiteto unaohusisha kilimo cha Ekari 5,000.
Amesema katika mradi huo wataboresha miundombinu ya kilimo kwa kuanzisha umwagiliaji wa kisasa, uzalishaji wa chakula ambapo kitajengwa kiwanda cha uzalishaji wa unga wa mahindi.