May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wiki ya Msaada wa Kisheria yazinduliwa Z’bar

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema kuwa imetengeneza idara maalum inayoshughulika na masuala ya msaada wa kisheria kwa ajili kutatua changamoto zinazowakumba wananchi wake wengi hususani wanawake, ambao wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo ndoa, mirathi, na ukatili, hali inayowalazimu kutafuta huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi, na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria, ambayo yamefadhiliwa na Shirika la Legal Services Facility (LSF) mwaka huu 2021, huku yakiwa na kauli mbiu ya “Msaada wa kisheria ni chachu ya kumuwezesha mwanamke kiuchumi.”

Waziri Suleimani amesema kuwa, maadhimisho hayo yana lengo la kuwezesha utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi wote ingawaje kauli mbinu ya mwaka huu inawalenga wanawake, kwasababu asilimia kubwa ya watu wanaonyimwa haki katika maeneo mengi cnhini ni wanawake.

“Kwa muda mrefu serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali zinazolenga kujenga ustawi wa haki za wanawake na Watoto nchini. Mathalani, tumeanzisha mahakama ya udhalilishaji ili kuangalia masuala ya udhalilishaji kwa watoto na wanawake ili kutoa adhabu zinazostahili kwa watuhumiwa,” amesema Waziri huyo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Legal Services Facility – LSF Bi Lulu Ng’wanakilala akiongea wakati wa uzinduzi wa wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar inayofadhiliwa na LSF na kuratibiwa na Ofisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi na Utawala Bora itakayowawezesha wananchi visiwani Zanzibar kupata elimu na msaada wa kisheria kupitia program maalumu zitakazoendeshwa kwa wiki nzima Unguja na Pemba.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Bi.Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa taasisi yake inaona fahari kuwa sehemu ya mafanikio ya maadhimisho ya wiki ya sheria visiwani Zanzibar kwakuwa sherehe hizo zinalenga kuhamasisha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wenye uhitaji ikiwemo wanawake na Watoto.

LSF ambalo ni shirika lisilo la kiserikali linalofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) pamoja na Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) limetoa kiasi cha shilingi milioni 27 kufadhili maadhimisho ya wiki ya sheria visiwani Zanzibar mwaka 2021.

“Pamoja na kuwezesha maadhimisho yam waka huu visiwani Zanzibar, LSF kupitia uwezeshaji wakisheria tumekuwa tukifanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kwa wananchi wote hasa wanawake kwa kutoa ruzuku katika mashirika takribani 200 yanayotoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria zaidi nchi nzima.” amesema Mtendaji mkuu wa LSF.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi na Utawala Bora, Mh. Haroun Ali Suleiman pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Legal Services Facility – LSF Bi Lulu Ng’wanakilala wakizindua rasmi wiki ya Msaada wa kisheria Zanzibar inayoanza leo tarehe 7 hadi 12 Juni 2021 visiwani Zanzibar.

Akinukuu ripoti ya mwaka 2020 iliyochapishwa na LSF inaonyesha kuwa wanawake wamekuwa ndio kundi kubwa linalohitaji zaidi msaada wa kisheria kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumbani na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Ng’wanakilala ameongeza kuwa ripoti yao inaonyesha kuwa, katika kila matukio (4) ya ukatili yaliyoripotiwa na wanawake mwaka yalihusisha unyanyasaji wa kijinsia, ambapo visa vyote vilivyoripotiwa vinakadiriwa kufikia asilimia 26.5 kwa mwaka 2020.

“Hii inaonyesha iko haja ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii kulinda na kutetea haki za makundi mbalimbali hususani wanawake na tunaamini wiki hii itatoa fursa kwa wananchi wa Zanzibar kupata huduma za msaada ya kisheria pamoja na elimu itakayochochea upatikanaji wa haki,”ameongeza.

Wiki ya msaada wa kisheria visiwani Zanzibar imeziduliwa leo Juni 7, 2021 na inatarajiwa kufikia tamati Jumamosi Juni 12, 2021, ambapo itaandamana na shughuli ya utoaji tuzo kwa wadau mbalimbali wanaochangia katika sekta ya msaada wa kisheria ikiwa ni njia ya kuthamini mchango wao muhimu katika maendeleo ya taifa kwa ujumla.