June 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Wahimizwa Kutafuta Ushauri wa Kisaikolojia kwa Wataalamu


Na Joyce Kasiki,Timemsmajira online,Dodoma


Chuo cha Ustawi wa Jamii kimewahimiza wananchi kutafuta huduma za ustawi wa jamii na ushauri wa kisaikolojia kutoka kwa wataalamu wenye sifa stahiki ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na ushauri usio sahihi unaotolewa na watu wasiokuwa na taaluma husika.


Akizungumza Juni 21,2026 katika maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Joyce Nyoni, alisema wananchi wanapaswa kutumia huduma zinazotolewa na maafisa ustawi wa jamii waliopo katika ngazi za kata na mitaa pamoja na vituo vya kitaalamu.


Alisema changamoto za maisha ni jambo la kawaida kwa kila mtu, lakini uwezo wa kukabiliana nazo hutofautiana, hivyo wataalamu wa ustawi wa jamii na saikolojia wana nafasi muhimu ya kuwasaidia wananchi kujenga uwezo wa kuzitambua na kuzikabili kwa njia sahihi.
Kwa mujibu wa Dkt. Nyoni, kupata ushauri kutoka kwa watu wasio na utaalamu wa kutosha kunaweza kusababisha hali ya mhitaji kuwa mbaya zaidi, hasa kwa watu wanaokabiliwa na changamoto za afya ya akili na msongo wa mawazo.


Aidha, alisema Chuo cha Ustawi wa Jamii kinaendelea kuandaa na kuzalisha wataalamu wa ustawi wa jamii na ushauri wa kisaikolojia kupitia programu mbalimbali zinazolenga kukidhi mahitaji ya jamii na taasisi za umma.
Alitaja baadhi ya programu hizo kuwa ni Shahada ya Ustawi wa Jamii pamoja na Shahada ya Ushauri Nasaha na Saikolojia, ambazo zimeendelea kuzalisha wataalamu wa kutoa huduma za kijamii na kisaikolojia nchini.


Dkt. Nyoni alisema wanafunzi wa chuo hicho hupata mafunzo ya nadharia na vitendo kupitia kituo cha huduma za kisaikolojia cha chuo pamoja na ushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na maeneo yaliyokumbwa na maafa.
Alieleza kuwa ushiriki wa chuo hicho katika Wiki ya Utumishi wa Umma unalenga kutangaza programu za masomo, kutoa huduma za udahili na kuhamasisha wananchi kutumia huduma za elimu, ushauri na msaada wa kisaikolojia.


Pia alisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika wataalamu wa ustawi wa jamii na afya ya akili ili kujenga jamii yenye ustawi, uwezo wa kukabiliana na changamoto na kufikia maendeleo endelevu.
Xxxxxxx