May 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Rukwa wahimizwa kupiga kura

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Rukwa

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amewataka wananchi 638,979 wa vijiji vyote 339, mitaa 167, kata 96, tarafa 16, halmashauri nne na wilaya tatu mkoani hapa walioandikishwa kwa ajili ya kupiga kura, kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu utaofanyika Oktoba mwaka huu.

Wangabo pia amewakumbusha wakulima kuwa katika kipindi hiki cha kampeni, wasisahau kuandaa mashamba yao kwa ajili ya msimu wa kilimo wa mwaka 2020/21 na kusisitiza kuwa wananchi wasiegemee sana siasa wakasahau maisha ya kawaida, ambayo ni kilimo kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Rukwa.

Mkuu huyo wa Mkoa ameyasema hayo juzi alipotembelea miradi ya Lipa kulingana na Matokeo EP4R na miradi ya afya na usafi wa mazingira (SWASH), inayotekeleza ujenzi wa madarasa na vyoo vya wananfunzi kwa shule za msingi na sekondari wilayani Kalambo ambapo wilaya hiyo, imepokea sh. 529,679,504 kwa mwaka huu wa fedha ili kutekeleza miradi hiyo.

Awali wakati akisoma taarifa ya miradi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Eric Kayombo amesema sh. 353,900,000 zimepokelewa katika shule saba za msingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo na sh. 175,776,504 zimepokelewa katika shule nyingine saba za msingi za ujenzi wa vyoo.

“Mkuu wa Mkoa, utekelezaji wa miradi hii umeanza mwaka huu wa fedha 2020/21 badala ya mwaka 2019/20, hii ni kutokana na halmashauri kupokea fedha za miradi mwishoni mwa mwaka wa fedha 2019/20 na kufanya kuvuka mwaka na kuanza kutekeleza mwaka huu wa fedha, miradi ya EP4R ipo katika hatua za msingi na miradi ya afya na usafi wa mazingira, ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji,” amesema.

Wangabo alitoa miezi miwili kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, kuhakikisha wanamaliza miradi hiyo kwa shule za msingi na sekondari ili kuimarisha miundombinu ya shule hizo, ambazo miradi hiyo inatekelezwa ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana Matai, ambayo inatarajiwa kuanza kupokea wananfunzi kuanzia mwaka 2021.

%%%%%%%%%%%%%%%