April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kushoto) akimsikiliza mkazi wa Kijiji cha Matela, Naombi Mbotela akieleza adha waliyokuwa nayo kabla ya kujengewa mradi wa maji.Picha na Mohamed Saif

Wananchi Magu wamshukuru Rais Magufuli

Na Mohamed Saif, Magu

WANANCHI wa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wamemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwaondolea kero ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma ya majisafi na salama.

Shukrani hizo zimetolewa juzi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Maji,Jumaa Aweso ya kukagua mradi wa maji wa Matela katika kijiji cha Matela wilayani humo.

Awali, Aweso alisema ziara yake imelenga kutembelea miradi ambayo wakandarsi wake wamechelewa kuikamilisha kwa wakati kama inavyoelekeza mikataba yao.

Wananchi wa Kijiji cha Matela, Wilayani Magu wakifurahia mradi wa maji wakati wa ziara ya Naibu waziri wa Maji, Jumaa Aweso (hayupo pichani) kwenye mradi huo

Alibainisha kuwa Matela ni miongoni mwa miradi uliyoisumbua Wizara ya Maji kwani ujenzi wake ulichukua muda mrefu na hivyo kuwacheleweshea wananchi kupata huduma ya maji kinyume na azma ya Rais Dkt.Magufuli.

“Tangu anaingia madarakani, Rais Magufuli aliazimia kuwaondolea kero ya maji wananchi wake, kuna baadhi ya miradi inakwamisha azma hiyo kufikiwa kwa wakati ukiwemo huu wa Matela ambao hata hivyo nafarijika kuona sasa nao umekamilika,” alisema Aweso.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Naibu Waziri Aweso, wananchi wa Matela walisema licha ya kwamba mradi huo umechelewa kukamilika kwa wakati lakini umeleta faraja katika maisha yao.

Naomi Mbotela, Mkazi wa kijiji cha Matela alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia mradi huo ambao alisema umewaondolea kero ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kufuata huduma ya maji.

“Kwa sasa hatuna shaka kwenye suala la maji,zamani sisi wanawake tuliteseka sana, tulikua tunatoka Saa 11 alfajiri na kutembea umbali mrefu kufuata maji na hii wakati mwingine ilitusababishia migogoro kwenye ndoa zetu,” alisema Mbotela.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Matela, Elias Njita alisema uwepo wa mradi huo ni uthibitisho kuwa Rais. Dkt Magufuli ni Rais wa wanyonge.

“Tunamshukuru sana Rais kutuona na kutujali sisi wanyonge huku vijijini, ametoa fedha nyingi kutujengea huu mradi ili sisi wanyonge tupate maji,” alisema Njita.

Aliahidi kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli hasa ikizingatiwa kwamba kwa muda mrefu wananchi wa maeneo ya vijijini wamekuwa wakisahaulika.

“Tunaahidi sisi tutamuunga mkono Rais, tunaahidi hatutomuangusha kazi anayofanya ni kubwa na ni ngumu sisi wanyonge tulikua tumesahaulika lakini yeye anatujali ili na sisi tuweze kujikwamua kimaendeleo,” aliongeza Njita.

Aidha, kwa mujibu wa msimamizi wa mradi Meneja wa Wakala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilayani Magu, Mhandisi Anna Mbawala ni kwamba ulianza kutekelezwa na Mkandarasi M/S STC Construction Company Ltd Mwaka 2017 na ulipaswa kukamilika 2019 na kuwa umetekelezwa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) kwa gharama ya shilingi milioni 397.9.

Alibainisha kwamba ulianza kutoa maji rasmi tarehe 02 Agosti, 2020 na kuwa umekabidhiwa kwa Jumuiya ya watumiaji maji ya Nyanguge-Muda kwa ajili ya kuhudumia wakazi wapatao 5,000 wa Kijiji cha Matela na vitongoji vyake.