May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hati 297 zakabidhiwa kwa Walimu

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

JUMLA ya hati za viwanja 297 zimekabidhiwa kwa baadhi wa walimu ambao ni walengwa wa mradi wa Viwanja vya Makazi ya walimu katika eneo la Nyamiswi Kata ya Sangabuye wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Mradi huo wa umilikishaji wa viwanja vya makazi kwa gharama nafuu kwa walimu wa shule za sekondari na msingi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ulianza Februari 2019, kutokana na wazo la Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo John Wanga.

Pia mradi huo ni moja ya motisha kwa walimu kutokana na juhudi walizofanya katika ufundishaji na kuwawezesha wanafunzi wa Wilaya ya Ilemela kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa kwa darasa la saba, kidato cha nne na sita mwaka 2018.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Ilema iliyoenda sambamba na zoezi la kuwakabidhi walimu hao pamoja na wananchi wa kada mbalimbali hati, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula, amesema, wakati wanaanza mchakato huo wengi waliona kama utani na hii imetokana baada ya walimu hao kufanya kazi nzuri na kuleta heshima kwa Halmashauri hiyo kwa kushika nafasi ya sita kitaifa kwenye matokeo ya shule za msingi na kwa heshima ya walimu pamoja na kuwalipa fadhira waliona wawe na namna ya kuwaandalia utaratibu wa kuwapatia viwanja vyenye hati kwa gharama nafuu ili waweze kuwa na makazi yao.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akimkabidhi hati ya kiwanja kwa mmoja wa walimu ambao ni miongoni mwa wanufaika wa mradi wa viwanja vya Makazi ya walimu wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. Picha na Judith Ferdinand.

“Ilikuwa kama ndoto lakini leo naona kama imetimia, ni suala la kumshukuru Mungu na kwamba ukimtumaini yeye katika mipango unayoipanga anauwezesha bila wewe kujua, wakati tunaanza mchakato huu wengi waliona kama utani na kuwa hatutofanikiwa, lakini nimshukuru sana Mwenyekiti wa Chama cha Walimu(CWT) pamoja na Katibu wake,baada ya kuwaingizia wazo hili walilipokea moja kwa moja na kuanza utaratibu wa kuwapanga walimu(kuwaorganize),” amesema Dkt. Angeline.

Amesema, kama kuna watumishi wa kada nyingine pia wanataka viwanja kwa namna hiyo basi nao wajipange kama walivyofanya walimu kwa kuanza utaratibu wa kuchangia fedha kiwango kinachotakiwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wa Halmashauri hiyo Shukrani Kyando, amesema katika zoezi hilo Naibu Waziri wa Ardhi huyo amegawa hati 1,569 na kati ya hizo 1,254 ni za maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo.

Huku 315 ni za mradi wa walimu na watumishi wa afya waliopimiwa eneo la Nyamiswi ambapo miongoni mwa hizo hati 297 ni za walimu na 18 za watumishi wa afya na katika kipindi cha miezi minne Halmashauri hiyo imetoa hati 6061 huku tangu mwaka 2016 imepima viwanja 59,000 na kumilikisha viwanja 31,000.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo Mwalimu wa shule ya msingi Gedeli, Elijaneth Moshy ameshukuru Rais kwa kumteua Naibu Waziri huyo ambaye ameweza kubuni jambo hilo la kuwaheshimisha walimu kwa kuweza kupata hati kwa ajili ya kujenga nyumba katika maeneo rasmi hivyo hiyo ni fursa hata wakistafuu kuishi maisha mazuri huku Halmashauri nyingine nchini ziweze kuanzisha mradi kama huo ili kuwezesha walimu na watumishi wengine kuwa na uhakika wa maisha hata watakapo stafu.

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Ziwa Baraka Ladislaus, amesema benki hiyo inatoa mikopo ya ujenzi wa nyumba kwa mtu mwenye hati ya kiwanja,hivyo ipo tayari kushirikiana na walimu kuwapatia mkopo kwa ajili ya kujenga nyumba ambao unalipwa taratibu kwa kipindi cha miaka 15.

Kwa upande wake Katibu wa kamati ya viwanja vya walimu Manispaa ya Ilemela Albert Mahuyu amesema, jumla ya viwanja 525 kwa ajili ya umilikishwaji wa walimu vimepimwa na kutokana na juhudi za kuhamasisha walimu kuhusu malipo jumla ya milioni 606 zimekusanywa na kuwekwa kwenye akaunti ya kamati sawa na gharama za viwanja 404 huku changamoto ikiwa ni baadhi ya walimu kutokamilisha malipo.