May 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahabari washauriwa kuelimisha jamii utekelezaji miradi ya TASAF

Na Joyce Kasiki, Dodoma

KATIBU Tawala wa mkoa wa Dodoma, Kessy Maduka amewataka wanahabari kuendelea kuelimisha jamii wananchi hususan wa kipato cha chini ambao miongoni mwao kuna walengwa wa Mfuko wa Kusaidia Kaya masikini (TASAF) ili wafanye kazi kwa bidii kupiga vita umasikini.

Maduka ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kwa wanahabari wa Mikoa ya Dodoma,Singida,Iringa na Shinyanga iliyolenga kuongeza uelewa kwa kundi hilo kuhusu utekelezaji awamu ya pili cha ya tatu TASAF.

“Hivi karibuni nchi yetu imeingia kwenye uchumi wa kati na kila Mtanzania anataka kuona tafsiri ya kuingia kwenye uchumi huo moja ya sababu zilizochangia ni maendeleo yetu katika kuongeza uzalishaji na kupiga vita umasikini.” Amesema Maduka.

Amefafanua kwamba vyombo vya habari vina nguvu katika kujenga ushawishi kwa jamii na vina nafasi kubwa katika kuleta matokeo chanya katika jamii kama vitatumika vizuri na vinaweza kuleta matokeo hasi kama havitatumika vizuri.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TASAF, Ladislaus Mwamanga amesema lengo la kikao kazi hicho ni kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu miradi ya TASAF, kwa kuwa ni kundi muhimu katika utekelezaji wa shughuli za mfuko.

Aidha amesema zaidi ya shilingi trilioni mbili zitatumika katika mradi huo na kwamba kaya zitakazohudumiwa ni takriban 800,000.

Ameongeza kuwa baada ya uchaguzi TASAF itaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo wabunge na makundi mengine katika ngazi za chini ili kuwezesha kila mmoja kutambua nafasi yake katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha malengo yanafikiwa.