May 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahabari wahimizwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

RAIS wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewataka wanahabari nchini kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kujenga umoja na kulinda maslahi yao mahali pa kazi.

Nyamhokya ameyasema hayo leo Mei 25 wakati akizungumza katika mafunzo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya JOWUTA na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Amesema umoja kupitia vyama vya wafanyakazi utasaidia wanahabari kuwa na sauti ya pamoja katika kupigania haki zao pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama hivyo ili kuimarisha nguvu ya wafanyakazi nchini.

“Vyama vya wafanyakazi vina mchango mkubwa katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao na kutetea maslahi yao wanapokumbwa na changamoto kazini,” amesema Nyamhokya.

Amesema wanahabari wengi nchini wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu bila mikataba rasmi ya ajira huku wengine wakilipwa kwa kutegemea idadi ya habari wanazoandika, hali inayowanyima uhakika wa maisha pamoja na mafao muhimu ya kazi.

Aidha, amesema umoja ni silaha muhimu katika kupambana na unyanyasaji wa kikazi na ukosefu wa haki kwa wafanyakazi.

Katika hatua nyingine, Nyamhokya ameipongeza WCF kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa mfuko huo kwa wafanyakazi mbalimbali nchini, akieleza kuwa bado kuna wafanyakazi wengi wasiofahamu namna mfuko huo unavyoweza kuwasaidia wanapopata madhara au ajali zinazotokana na kazi zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma, amesema ushirikiano kati ya chama hicho na TUCTA umeanza kuzaa matunda tangu JOWUTA ilipopokelewa rasmi ndani ya shirikisho hilo mwaka jana mjini Singida.

Amesema hatua hiyo imeongeza nguvu ya chama hicho katika kupigania maslahi ya wanahabari nchini.

Juma amesema zaidi ya asilimia 80 ya wanahabari nchini hawana mikataba rasmi ya kazi licha ya baadhi yao kuwa na elimu kubwa ya taaluma mbalimbali, hali inayowafanya kukosa haki za msingi za wafanyakazi na kutotambulika rasmi na waajiri wao.

Aidha, amesema chama hicho kinaendelea kushirikiana na Wizara ya Kazi pamoja na Kamishna wa Kazi kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanahabari zinapatiwa ufumbuzi, ikiwemo suala la mikataba ya ajira na mazingira bora ya kazi.