May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahabari Afrika washauriwa kusaidia juhudi za maendeleo

Na Jackline Martin, Timesmajira Online, Arusha

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka wanahabari kutumia kalamu zao kukabiliana na changamoto zilizopo nchini na barani Afrika juu ya rasilimali zinazoharibiwa ili tatizo liweze kutatuliwa

Aliyasema hayo wakati akizindua maonesho kuelekea kilele cha siku ya Uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo yatafanyika Mei 5, mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema wajibu wa sekta ya habari ni kusaidia bara la Afrika, rasilimali zilizopo zibadilike kuwa baraka kwa watu wake ili kuona matokeo ya rasilimali hizo.

Alisema wakati umefika kwa wanahabari kuchukua maamuzi ya kusaidia bara hilo kufaidika na rasilimali zake na watu wake wajivunie kuwa Waafrika na wajivunie kuwa kwenye bara lenye rasilimali za kutosha.

“Tukipewa hesabu ya rasilimali tulizonazo na ukilinganisha na mabara mengine hatupaswi kuwa hapa tulipo, lakini kila mmoja wetu anapaswa kutimiza wajibu wake na wanahabari tunalo jukumu hilo kubwa la kubadilisha mambo maana hayapo sawa,” alisema Nape na kuongeza;

“Angalia maovu mengi yaliyopo kwenye bara la Afrika sehemu ambapo kuna rasilimali nyingi ndipo watu wanapogombana zaidi na sehemu ambapo kuna rasilimali za kutosha ndipo watu wake wanapoteseka sana, sasa umefika wakati wa waandishi kusimama kusaidia kubadilisha mambo hayo, “alisisitiza waziri huyo.

“Hapa nchini kwetu sheria zinatungwa na Bunge, nichukue nafasi hii kumpongeza Spika wa Bunge kwa utayari wake alionieleza kuwa wanasubiri tukamilishe mapendekezo ya mabadiliko ya sheria, leteni tufanye mabadiliko ili tasnia ya habari iende kwa kasi, hivyo Bunge lipo tayari sisi tukamilishe kwani bunge letu lina kazi ya kutunga na kufuta sheria zinazokwaza ukuaji wa sekta mbalimbali, “alisema Waziri huyo.

Alisema anatumai waandishi watatumia fursa nyingi katika kujadili na kutafuta njia bora za kushughulikia na kukabiliana na changamoto zinazowakumba, huku wakiainisha fursa zilizopo katika kuendeleza sekta ya habari barani Afrika.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Jim Yonazi alisema kupitia mkutano huo sekta ya habari inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi na kuchagiza uhuru wa vyombo vya habari Duniani.

“Sekta ya habari inaendelea kuchangia vyema katika ukuaji wa uchumi wa nchi na pato la taifa kupitia mitandao ya kijamii,”

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Ruben alisema uandishi wa habari ni jambo linalogusa jamii na kuleta maendeleo katika jamii na nchi kwa ujumla.

Mkurugenzi mtendaji umoja wa vyama vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Abubakari Hassan alisema dunia imebadilika na vitu vingi vimehamia kwenye mitandao ya kijamii, hivyo aliwataka waandishi wote kutumia vyema mitandao hiyo ili kufanya jamii iwe na uelewa mpana wa kile kinachoendelea na kuweza kupata mambo muhimu ya kihabari