May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheikh Kabeke awahimiza wananchi kujitokeza katika sala ya Eid uwanja wa Nyamagana

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke,amesema sala la sikukuu ya Eid kimkoa itafanyika katika uwanja mkongwe wa Nyamagana uliopo wilayani Nyamagana mkoani Mwanza,hivyo ametoa wito kwa waumini wa kiislamu kujitokeza kwa wingi.Huku akiwapongeza Wafanyabiashara jijini Mwanza kwa kuuza bidhaa bei ya kawaida katika kipindi chote cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumza mkoani hapa na waandishi wa habari, Sheikh Kabeke,amewashukuru watanzania wote kwa kuheshimu na kuungana katika kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani huku akiwasisitiza waumini wa dini hiyo kujitokeza kwa wingi kuhudhuria sala hiyo itakayofanyika kimkoa katika uwanja wa Nyamagana.

Pia ametumia fursa hiyo ,kuwahimiza waumini wa dini hiyo kuendeleza yale matendo mema waliofanya katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Ndani ya Ramadhani tumesali sala tano,tunewahurumia watu,niwaombe waislamu matendo hayo tuendelee nayo yale tuliojifunza ndani ya Ramadhani katika siku 29-30,yaendelee baada ya Ramadhani tutaishi ni aibu kubwa siku ya kwanza ya pili unakutwa mtaroni umelewa kwani tusiendelee kutoa sadaka na kutenda mema,” amesema Sheikh Kabeke.

Naye Mwennyekiti wa Soko Kuu la Mwanza Hamad Nchola,amesema bidhaa kuelekea katika sikukuu ya Eid El fitr bei ni ya kawaida licha ya kuwa imepanda kutokana na vita inayoendelea nchini Ukrein.

Hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara kutopandisha bei ya bidhaa kwa sababu ya sikukuu ya Eid huku wananchi waende kununua bidhaa katika soko hilo kwani bei zake ni zakawaida Nao baadhi ya wafanyabiashara Jijini Mwanza akiwemo Eva Kelvin,amesema mwaka huu biashara siyo nzuri ukilinganisha na miaka mingine.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ramadan Ng’anzi akitoa taarifa kwa vyomba vya habari amesema,katika kuelekea Sikukuu ya Eid –Elfitr jeshi hilo Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limejipanga vyema katika kuhakikisha sherehe za sikukuu ya Eid –Elfitri zinasheherekewa kwa amani na utulivu.

“Tuwatoe hofu wananchi kwani ulinzi umeimarishwa,katika nyumba za ibada misikitini ulinzi umeimarishwa vyakutosha kwani Askari watakua wakipita kwa doria za miguu, pikipiki na magari katika maeneo yote ya Jiji na Mkoa wa Mwanza,pia niwatake wananchi wanapokwenda kwenye nyumba za ibada au kumbi za starehe wasiache nyumba zao bila uangalizi au kiziacha wazi kwani kunaweza kushawishi wezi kuiba,” amesema Ng’anzi.

Pia ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa pamoja na kusherekea sikukuu hiyo wasisahau majukumu yao ya kuwa makini na watoto wao kwa kutowaacha peke yao barabarani na katika sehemu za michezo mfano maeneo ya beach/mialo na kwenye bembea, hata hivyo disco toto ni marufuku.

Vilevile amesema ni marufuku kwa madereva wa vyombo vya moto kuendesha wakiwa wamelewa au mwendo kasi, endapo ikibainika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Mwanza juu ya Sala ya Eid ambayo kimkoa itafanyika uwanja wa Nyamagana uliopo wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.(picha na Judith Ferdinand)
Mwenyekiti wa Soko Kuu la Mwanza Hamad Nchola, akizungumza na waandishi wa habari juu ya bei ya bidhaa kuelekea sikukuu ya Eid.(picha na Judith Ferdinand)