April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi Ebenezer watoa ombi serikalini

Na Hadija Bagasha, Tanga

RAIS Samia Suluhu ameombwa kuboresha sekta ya elimu na kupigania haki za wanafunzi ili mwanafunzi anapomaliza awe na ufahamu wa kuwa na elimu ya biashara ambayo itamsaidia kuwa na ufahamu wa shughuli za kuongeza kipato na pindi atakapofanikiwa kimasomo aweze kuwa na mbinu za kuvutia wawekezaji.

Ombi hilo limetolewa na wanafunzi wanaohitimu darasa la saba katika shule ya Ebenezer English Medium iliyopo jijini Tanga.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wanafunzi hao, Jasmine Hassan alisema kuwa iwapo wizara ya elimu itaimarishwa itasaidia kupanua wigo mpana wa watanzania wengi kunufaika kupitia sekta hiyo.

Alisema kuwa, sekta hiyo itakapoboreshwa itasaidia kufungua milango ya wawekezaji hapa nchini na kuweza kuingia katika soko la ushindani wa kibiashara na mataifa mengine.

“Iwapo leo hii nikipata nafasi ya kukutana na Rais Samia jambo kubwa atakalomueleza ni kuboresha sekta ya elimu kwa kuzidi kutoa policy nzuri za biashara ili kuzidi kuleta wawekezaji zaidi nchini mwetu ili kuifanya Tanzania kuzidi kuleta maendeleo katika taasisi ya elimu ili kuwasaidia watu wengi kupata elimu, “alisistiza Jasmine huku akisema anajivunia kupata Rais mwanamke.

Mmoja wa wanafunzi wengine, Rill David alimpongeza Rais Samia kwa kuwa ndiye mwanamke wa kwanza kuongoza nchi hii wakiamini kuwa nchi haitoyumba na badala yake itanyooka wakati wote kwani kwenye maendeleo ya mwanaume mwanamke yupo nyuma yake.

“Nilibahatika hata leo kumuona nitamsisitiza kudumisha na kuimarisha taasisi za elimu ikiwemo kupigania haki za wanafunzi pamoja na wanawake,”alisema David.

Katika mahafali hayo Mkurugenzi wa mtendaji wa shule ya Ebenezer na Mwambani, Ebenezer Issack Mlangwa alisema kuwa shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kwa kuongoza katika matokeo yake ya darasa la saba tokea mwaka 2015 kimkoa hadi kitaifa.

Mkurugenzi Mlangwa alisema kuwa silaha kubwa wanayoitumia shuleni hapo ni pamoja na kumshirikisha Mungu katika kila hatua lakini pia nidhamu na maadili mema waliyowajengea wanafunzi wao huku akiwataka wanafunzi hao wanaohitimu kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi katika mitihani yao wanayotarajia kuifanya hivi karibuni.

“Msingi wa maadili wanayopata hapa shuleni ni nyenzo kuu ya kuhakikisha wanafunzi wetu wameiva na wanajua nini wanatakiwa kufanya katika ulimwengu tulio nao hivi sasa, “alisistiza Mkurugenzi Mlangwa.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Joseph Kilonzo alisema kuwa zimebakia wiki mbili wanafunzi kufanya mtihani wao wa taifa wa kuhitimu darasa la saba hivyo wamewaanda vya kutosha wanafunzi hao katika kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye matokeo yao ya NECTA.