May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi 1,092,984 wachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2024

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online Mwanza

Jumla wanafunzi 1,092,984 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2024 huku idadi ya waliofaulu kujiunga ikiwa imeongezeka kwa asilimia 1.57 ikilinganishwa na mwaka 2023.

Hayo yamebainishwa leo Desemba 17,2023 na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa wakati wa mkutano wake na wataalamu wa Sekta ya Elimu pamoja na waandishi wa habari uliofanyika uliofanyika mkoani hapa.

Ambapo ameeleza kuwa uchaguzi ulihusisha wanafunzi 1,092,984 wakiwemo Wasichana 507,933 na Wavulana 585, 051 ambao walifaulu mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2023.

Mchengerwa ameeleza kuwa idadi ya wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza Januari, 2024 imeongezeka kwa wanafunzi 16,947 sawa na ongezeko la asilimia 1.57 ikilinganishwa na wanafunzi 1,076,037 waliopata alama za kuwawezesha kujiunga na kidato cha kwanza mwaka, 2023.

Ameeleza kuwa kati ya waliofaulu na kupangiwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari, 2024 wamo wanafunzi wenye mahitaji maalum 3,587 ambapo wasichana 1,590 na wavulana 1,997.

Sanjari na hayo amewataka Wakuu wa mikoa na Wilaya kusimamia suala la wanafunzi hao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza muhula mpya wa masomo wa mwaka 2024 unaoanza Januari 8 mwakani wanaripoti shuleni kwa wakati na kwamba taarifa zote za wanafunzi na fomu za kujiunga zinapatikana www.tamisemi.go.tz na www.necta.go.tz.