May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waliofutiwa matokeo kurudia mtihani

Na Irene Clemence TimesMajira Online

BAADA ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wazazi na walezi wa watahiniwa 2,194 waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) kwa sababu ya udanganyifu leo Disemba 10 Baraza la mitihani Tanzania (NECTA) limetagaza kurudiwa kwa mtihani huo tena ambao unatarajia kufanyika Disemba 21 hadi 22 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam Jijini Dar es salaam mapema leo Disemba 10 ,Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA, Athumani Amasi amesema baada ya matokeo kutangazwa, baraza hilo liliendelea kupokea malalamiko kutoa kwa wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wazazi na walezi wa watahiniwa waliofutiwa matokeo kwa sababu ya udanganyifu.

“Baada ya matokeo kutangazwa baraza la mtihani liliendelea kupokea malalamiko kwa wadau ambao walilalamika kuwa udanganyifu katika mtihani ulipangwa na kutekelezwa na uongozi wa shule husika , walimu na wasimamizizi wa mtihani ambao waliwapatia majibu ya mtihani”amesema Amasi

Na kuongeza kuwa “walidai

kuwa kwa kuzingatia umri wa watoto waliofutiwa matokeo wasingeweza kuyakataa majibu waliyopewa na walimu , wasimamizi wa mtihani,”alieleza Amasi

Aliendelea kueleza kuwa baraza limetafakari kwa kina malalamiko ya wadau kuona kuwa ni ya msingi na kuamua kuwapa fursa watahiniwa 2,194 waliofutiwa matokeo, kufanya mtihani wa marudio mapema kabla ya kusubiri hadi mwakani.

Hata hivyo amesema kwa watahiniwa ambao shule zao zimefungiwa kuwa vituo vya mtihani watafanyia mtihani wao katika vituo vya jirani na shule zao na ambao shule zao hazikufungiwa watafanyia kwenye shule za jirani.

“mitihani huu wa marudio utaendeshwa na kusimamiwa na kamati za uendeshaji mtihani za mikoa husika kwa kuzingatia kanuni na taratibu za uendeshaji wa mitihani ya kitaifa”

Amasi Pia alibainisha kuwa matokeo ya watahiniwa watakaorudia mtihani yatawasilishwa mapema katika mamlaka zinazohusika na uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 ili watakaofauli waweze kuanza masomo pamoja na wenzao Januari, mwakani.

Alitaja orodha ya vituo 24 vya kufanyia mtihani wa marudio wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu ni shule ya msingi Arusha,Sandali, Maweni,Nshambya, Kambarage,Rubondo,Mila, Turwa, Magu, Buhogwa , Kilabela,Bukongo, Masuguru, Maporomoko na Bombo.

Kwa upande wa Vituo vilivyofungiwa ni shule ya msingi ya Kadama(Geita), Rweikiza(Kagera),Kilimanjaro(Arusha), Sahare(Tanga), St. Anne Marie(Dar es Salaam), Ukerewe(Mwanza), Peace land(Mwanza), Karume(Kagera).Nyingine ni shule ya msingi Al-Hikma(Dar es Salaam), Kazoba(Kagera),Mugini (Mwanza), Busara(Mwanza), Jamia(Kagera),Winners na Musabe(Mwanza), Elisabene(Songwe), High Challenge ( Arusha),Tumaini(Mwanza), Mustlead(Pwani), Moregas (Mara),Leaders (Mara)Kivulini (Mwanza) na St. Severine(Kagera).

Awali, wanafunzi hao walifanya mtihani Oktoba 05 -06, mwaka huu,Tanzania Bara kwa kusimamiwa na kamati za uendejshaji mitihani za mikoa na halmashauri na matokeo kutangazwa na Baraza la Mitihani Desemba Mosi, mwaka huu.

Katika taarifa ya matokeo yaliyotangazwa, pamoja na mambo mengine, jumla ya watahiniwa 2,194 walifutiwa matokeo yao kwa sababu za kubainika kuwa walifanya udanganyifu katika mtihani huo kwa mujibu wa kifungu 30(2)(b) cha kanuni za mitihani 2016 kikisomwa pamoja na kifungu cha 5(2)(i) na (j) cha sheria cha NECTA sura 107.