May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mageuzi makubwa sekta ya elimu mwaka 2024/5

-Wahitimu kujengewa uwezo wa kujiajiri, Wizara ya Elimu kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa vijana

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

WIZARA ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia imetangaza kufanyika kwa mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini ambayo yatawezesha wahitimu kujengewa uwezo wa kujiajiri.

Ili kuweza kufanikisha mageuzi hayo pamoja na kutekeleza majukumu yake mengine, Wizara hiyo imeliomba Bunge kuidhinishiwa Wizara hiyo kiasi cha sh. trilioni 1.9 kwa mwaka wa Fedha 2024/25.

Hayo yalisemwa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2024/26.

Kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa Mpango wa Bajeti kwa Mwaka 2024/53, Prof. Mkenda alisema Wizara imepanga kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika.

Vingine ni vipaumbele vyenye kujielekeza katika kutegemeza tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu katika agenda ya maendeleo ya nchi.

“Mheshimiwa Spika, vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini,” alisema Prof. Mkenda.

Kipaumbele kingine kwa mujibu wa Prof. Mkenda ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu).

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda kipaumbele cha tatu kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu, nne kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuendeleza tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Aidha, alisema ni kuendelea na utekelezaji wa Sera na Mitaala, Mapitio ya Sheria na kuandaa Miongozo ya Utoaji Elimu na Mafunzo Nchini

Pia, alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala kwa ngazi ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Ualimu. Aidha, itaendelea na uandaaji wa zana za utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 ambazo ni Miongozo, Mfumo wa Kitaifa wa Tuzo na Sifa Linganifu (Tanzania Qualification Framework – TQF), Sheria na Kanuni, Mfumo wa Mtaala wa Kitaifa na Mfumo wa Tathmini wa Kitaifa katika ngazi ya Elimu ya Msingi, Sekondari, Ualimu, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Elimu ya Juu kwa lengo la kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa Sera.

“Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na maboresho ya mitaala ya elimu ya amali sanifu na elimu ya juu ili kuwezesha nchi kuandaa rasilimaliwatu yenye ujuzi na maarifa,” alisema.

Alisema katika kufikia azma hiyo, Serikali itafanya mapitio ya mitaala 171, kuandaa mitaala mipya 18, kuanzisha programu za vipaumbele 145 pamoja na matumizi ya mbinu bunifu za ufundishaji katika elimu ya juu.

Aidha, alisema itawezesha ziara za kimkakati kwa wafanyakazi wa sekta ya elimu katika nchi zenye uzoefu wa uandaaji wa rasilimaliwatu yenye maarifa na ujuzi wenye kuchangia katika ukuaji wa kati wa uchumi;

Pili alisema itasasisha na kuandaa mtaala mpya katika taasisi 17 za elimu ya juu na itahakiki mitaala 230 ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mipango ya nchi, soko la ajira la kitaifa na kimataifa na kuwawezesha wahitimu kujiajiri na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira,” alisema Prof. Mkenda.

Aidha, alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 kwa watendaji wa ngazi zote za elimu na mafunzo wakiwemo walimu wa shule za msingi; walimu wa shule za sekondari; wakufunzi wa vyuo vya ualimu.