May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIT kuanzisha kitengo cha mafunzo usafiri wa reli

Na Mwandishi Wetu 

CHUO cha Taifa Usafirishaji (NIT), kipo mbioni kuanzisha kitengo cha mafunzo ya usafiri wa reli mkoani Tabora kwa ufadhili wa Serikali ili kuendana na kasi ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika usafiri wa reli.

Aidha, chuo hicho kati ya Desemba mwaka huu na Januari mwakani kinatarajia kupokea ndege mbili za mafunzo ya upairoti hapa nchi na kitakabidhiwa rasmi na Serikali kwa ajili ya mafunzo ya anga.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Mkuu wa Chuo hicho, Dk Prosper Mgaya wakati wa kongamano la tisa la wahitimu wa chuo hicho ambapo kwa mwaka huu wa masomo watahitimu wanafunzi  2700.

Dk Mgaya amesema NIT wanajitaidi kutoa wanafunzi wenye weledi kwenye njia tano za usafirishaji, ambapo mwaka huu mada yao kuu ipo kwenye usafiri wa reli na wamefanya hivyo kwa sababu za kuzingatia Serikali inavyowekeza fedha nyingi katika usafiri wa reli.

Amesema ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ambao umefikia kwa asilimia 95, na kama mnavyoona mabehewa yameshaingia kwamba usafiri utaanza kutumika na pia Serikali imeshasaini mikataba ya ukimaliza kipande kilichobakia.

Naibu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt Prosper Mgaya akizungumza kwenye kongamano la tisa la wahitimu wa chuo hicho na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji kwa lengo la kuwakutanisha na wahitimu waliyomaliza NIT miaka ya nyuma.

“Na kama mlivyosikia Rais Dk Samia Suluhu Hassan amesema nchi yetu imekaa kwenye eneo la kimkakati ambayo nchi ya Congo na Burundi zinategemea nchi yetu ndiyo maana reli zitajengwa hadi kwenye hizo nchi ili tuweze kusafirisha mizigo kuja Tanzania,”

“Kwa umuhimu huu, chuo kipo mbioni kuanzisha kitengo cha mafunzo ya usafiri wa reli mkoani Tabora, kita fadhiliwa na Serikali na ndiyo maana chuo kinafanya ukaribu na shirika TRC kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa ajili ya kuanzisha hicho kituo,”amesema Dk Mgaya

Amesema kuwa ana amini ndani ya mwaka mmoja tayari mafunzo hayo yatakuwa yameanza, lakini sio hivyo tu pia wanategemea kupokea ndege mbili za mafunzo ya upairoti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Uthibiti wa Barabara kutoka  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Aridhini (Latra), Johansen Kahatano amesema chuo hicho kinaendelea kutanua wigo wa mitaala kwa kufikia maeneo mengi ya usafirishaji.

Naye mwanzilishi wa kongamano hilo, Injinia Dk Amaon Mwasandube amesema wanachojivunia ni kwamba wameshatoa wahitimu wengi kwenye sekta mbalimbali za usafirishaji na wamefanikiwa kusonga mbele.

“Kikubwa zaidi anaweza kujivunia hata upande wa usalama barabarani tumefundisha vijana wengi kozi za automobile na ukaguzi wa magari sasa hivi vijana wetu wengi ni ma RTO kwa sababu tulikuwa tunawafundisha pamoja na kozi maalum ya ukaguzi wa magari,”amesema