Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga Salum Nyamwese amewataka wananchi watakaopata huduma ya maji Mradi wa Maji Miji 28 kwenye wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani kuwa watulivu, kwani mradi unakwenda vizuri, na watapata maji Oktoba 31, 2026.
Akizungumza Agosti 12, 2026 mara baada ya kutembelea mradi huo unaojengwa kwenye Wilaya ya Korogwe, Nyamwese amesema amejiridhisha kwa kazi zinazofanywa na Mkandarasi, lakini pia na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) kuwa wanafanya kazi nzuri, na mradi umefikia asilimia 86.

Nyamwese amesema mradi huo Serikali imewekeza fedha sh. bil.171, na baada ya kupita kwenye chanzo cha maji (Dakio) kutoka Mto Pangani, na kutembelea Chujio vyote vilivyopo Kata ya Mswaha Darajani, na baadae kwenda kweñye tenki la Kwamatuku, wilayani Handeni, amejionea maendeleo makubwa yaliyofanywa kwenye mradi huo, hivyo akiamini shida ya maji ya muda mrefu hasa kwa wananchi wa Wilaya ya Handeni inakwenda kumalizika.
“Lengo la ziara hii, kwanza ni kuona mradi. Tulipopita ziara ya mwisho, na sasa hivi, tumeona mabadiliko, na kweli kazi inafanyika, na Mkandarasi amenieleza mradi umefika asilimia 86, na kazi zilizobaki ni kuweka kuta eneo la mradi na umeme. Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani vifaa vingi vya umeme vimeshalipiwa, na vimeingia nchini. Kulikuwa na changamoto ya vifaa hivyo kupata msamaha wa kodi, lakini Wizara ya Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) na Wizara ya Maji wameweza kushirikiana kwa haraka na kupata msamaha wa kodi.

“Na ahadi tuliyopewa leo kufikia tarehe 31, Oktoba, mwaka huu, maji yatakuwa yamefika kwenye wilaya zetu. Kwa hiyo niendelee kutoa rai kwa wananchi wetu wa Handeni, Korogwe, Pangani na Muheza, tuwe watulivu, mradi wetu unaendelea vizuri, na tutapata maji safi na salama kwenye mabomba yetu. Wakandarasi na HTM wametuhakikishia hilo, na sisi hatuna wasiwasi nao. Huu mradi ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, ni matumaini na faraja kwa wananchi na hasa sisi wananchi wa Handeni” amesema Nyamwese.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HTM ambao ndiyo Wasimamizi wa Mradi huo, Robert Mtatiro, amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya, na wananchi wa Wilaya ya Handeni na miji ya Korogwe, Muheza na Pangani kuwa watapata maji ifikapo mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu.



More Stories
Kituo cha Saratani kuwa kimbilio kwa wananchi Mbeya
Waziri Kabudi:Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Lukuvi
Mkenda:Ujuzi agenda kuchochea ajira kwa vijana