March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walemavu waomba serikali kupanua wigo soko la viatu

Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya

SERIKALI imeombwa kupanua wigo wa soko la viatu hapa nchini ili kuongeza tija ya hususani kwa viatu vinavyotengenezwa na wajasiriamali wazawa wakiwemo watu wenye ulemavu.

Pia imeshauriwa mchango mkubwa wa Halmashauri ambao imekuwa ikitoa kwa wajasiriamali ikiwemo kuwapa mikopo ya fedha kwa makundi maalumu ikiwemo watu wenye ulemavu ni mzuri kwakuwa hauna riba lakini ipo haja ya kuwasaidia kupata soko la uhakika la bidhaa wanazozalisha ili waweze kumudu gharama za uzalishaji ikiwemo ununuzi wa malighafi walizosema wanazinunua kwa bei ghali.

Akizungumza na TimesMajira, mkazi wa mji mdogo wa Mbalizi ambaye ni mlemavu wa miguu, Joseph Njole amesema kuwa, amekuwa akijishughulisha na ushonaji viatu na utengezaji viatu ambao umekuwa ukimwezesha kuendesa maisha yake.

Njole amesema, katika suala la utengenezaji na ushonaji viatu kuna changamoto ya soko na kwa asilimia kubwa ni ngumu kutokana na mazingira yaliyopo hivyo aliomba serikali kuwasaidia kutanua wigo wa soko la viatu vinavyotenezwa hapa nchini.

“Asilimia kubwa ya wateja tulionao ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na kidogo wa vyuo kwa sisi kama sisi ni ngumu kuhamasisha kuwa kila shule ivae viatu vinayotengenezwa hapa Tanzania ,tunaomba serikali walau ingetusaidia kutafuta masoko ya viatu vyetu na kuongeza tija ya viatu vyetu walau kuongea na taasisi za shule wawe wananunua viatu vinavyotengenezwa hapa nchini,” amesema mlemavu huyo.

Pia ameomba serikali kutoa ruzuku kwenye viwanda vidogo vidogo na Halmashauri inasaidia kutoa mikopo ambayo haina riba lakini kwa shughuli zao kunakuwa na changamoto kidogo kutokana na ununuzi wa vifaa ya kufanyia kazi kwa gharama kubwa na ukichukua mkopo mpaka kuja kurejesha gharama za vitendea kazi inachukua muda mrefu hivyo serikali iliangalie hilo walau kutoa ruzuku ili waweze kununua vifaa ya kisasa kwa ajili ya shughuli zao.

Akizungumzia kuhusu walemavu ambao wamekuwa wakiona ulemavu walionao hawawezi kufanya kazi, Njole amewataka kuondoa dhana hiyo na kusema walemavu wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kwamba mlemavu ukijiweka tofauti na mtu mwingine unadhoofika na kujiweka chini na huwezi kufikiri kujishughulisha kufanya kazi.

Aidha Njole ameshauri watu wenye ulemavu kuunda vikundi na kusajili ili waweze kupatiwa mikopo kwani ipo na serikali inajali.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Zena Kapama amesema kwamba, Halmashauri imekuwa ikiwasaidia watu wenye ulemavu kukaa kwenye vikundi na kuwa kwa sasa kuna mwongozo ambao unasaidia hata mlemavu mmoja akiwa peke yake anaweza kupata mkopo mkubwa ni kuwa na vigezo na kujishughulisha.

Akizungumzia changamoto kwa watu wenye ulemavu, Kapama amesema wamekuwa wakidhulumiana wenyewe kwa wenyewe kutokana na baadhi yao kutokuwa waaminifu.