May 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakuu wa Rasilimaliwatu kukutana Dodoma

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

OFISI  ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) imeandaa kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kinacholenga  kubadilishana uzoefu na kujadili namna bora ya kuboresha usimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma.

Akizungumza na waandishi wa habari,jijini hapa jana Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Juma Mkomi amesema  kikao hicho kitawakutanisha Wakurugenzi na Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Amesema kuwa kikao hicho kitaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Ulio Sikivu, Jumuishi, Wenye Matokeo na Uwajibikaji Kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

Kwa mujibu wa taarifa Mkomi kuwa kikao kazi hicho ni sehemu ya utaratibu wa kila mwaka ambapo amesema kwa mwaka huu kitafanyika kuanzia Juni Mosi hadi 3 2026 katika Ukumbi wa Mabele Hall, Jijini Dodoma.

“Washiriki wa kikao hiki watapata nafasi ya kujadili matumizi ya mifumo mbalimbali ya kidijiti ikiwemo e-Uhamisho, e-Watumishi, e-Utendaji, e-Mrejesho pamoja na HR Assessment kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji huduma serikalini kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,”amesema Mkomi.

Vilevile amesema , kikao hicho kitajadili mafanikio na changamoto zilizopo katika usimamizi wa rasilimaliwatu pamoja na kuweka mikakati bora ya kuboresha utendaji kazi katika taasisi za umma.

Aidha amesema kuwa Mgeni rasmi katika kikao hicho anatarajiwa kuwa Ridhiwani Jakaya Kikwete ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia rasilimaliwatu na utawala katika utumishi wa umma nchini.

Hata hivyo amesema OR-MUUUB imewataka washiriki wote kujisajili mapema kupitia mfumo wa TSMS kupitia tovuti husika huku akisema mwisho wa usajili ni tarehe 29 Mei 2026 saa 6:00 usiku.

Pia alitoa msisitizo, viongozi wote wanatakiwa kushiriki wenyewe wasitume wawakilishi kama ambavyo baadhi huwa wanafanya.