May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima watakiwa kuendana na mabadiliko

Na Esther Macha Timesmajira Online,Songwe

KITUO cha Utafiti wa zao la Kahawa (TACRI ) Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kimewataka wakulima kutumia mfumo wa kuotesha miti ya kahawa shambani na kuacha na mfumo waliokuwa nao awali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na Timesmajira Online,Meneja na Mtafiti wa TACRI Kanda hiyo Dismas Pangalasi amesema kuwa katika msimu huu wa kilimo wameweka mikakati ya kupiganisha na mikoa mingine ambayo inapata huduma kutoka kwenye kituo hicho.

Amesema kuwa kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi hususani kwa Kanda ya Mbozi Mkoa wa Songwe kuna kila sababu ya kuhamasisha wakulima kupanda miti ya vivuli kwenye miche ya zao kahawa.

Ambapo ameeleza kuwa kwa sasa inabidi waanze kwenda kwenye mfumo wa upandaji wa kahawa huku wanapanda miti kwenye mashamba yao kwani ina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mabadiliko ya tabianchi yanakwenda na hali ya hewa umefika wakati sasa wakulima kubadilisha mfumo wa kilimo waliokuwa wanatumia awali kwani sio sawa na wakati walionao sasa,”amesema Pangalasi.

Pia amesema kwa msimu wa mwaka 2022 kiwango cha joto kilikuwa kikubwa kwa wastani wa nyuzi 33 haijawahi kutokea katika kipindi cha miaka 30 iliyopita kwa hiyo ni ishara kuwa kuna mabadiliko ya tabianchi. Sanjari na hayo amesema kuwa kituo hicho kimezalisha miti mingi ya kivuli na misitu lakini watu wa Mbozi hawana utamaduni wa kupanda miti.

Hivyo amewataka WanaMbozi kupanda miti vinginevyo maeneo ya Mkoa huo yatabadilika na kuwa jangwa kuna mengine watashindwa kulima kahawa.Mkuu wa Wilaya ya Mbeya,Beno Malisa amesema kuwa zao la kahawa ni la msingi na Wizara ya Kilimo imeweka ajenda ya kukuza kilimo huku mkazo ni kurudi kwa wakulima.

“Ni muda sasa wa kuhamasisha wale waliokata tamaa kulima kahawa na kwenda kulima mazao mengine kurudi kwenye kahawa ili kuongeza idadi na ongozeko la fedha za kigeni ambayo inaweza kumwongezea kipato mkulima,”amesema mkuu huyo wa Wilaya.