September 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wa Mwani Zanzibar kunufaika huduma za kidijitali

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira

WAKULIMA wa mwani Zanzibar, ambao wengi wao ni wanawake, wanatarajiwa kunufaika na malipo ya kidijitali na huduma mbalimbali za kifedha kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mixx na Yas Business.

Ushirikiano huo, uliosainiwa jana Zanzibar, unalenga kutumia teknolojia kurahisisha malipo, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi, hususan kupitia programu ya Seaweed Socio-Enterprise.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga amesema ushirikiano huo unaendana na juhudi za kutumia teknolojia kuongeza fursa za kiuchumi na kurahisisha huduma kwa wananchi.

“Tunataka kuona wanawake na vijana wanaoshiriki katika shughuli za kiuchumi, hususan wakulima wa mwani, wanapata fursa ya kutumia teknolojia kwa manufaa yao.

“Ushirikiano huu utarahisisha huduma, kuongeza uwazi katika malipo na kuwafungulia wananchi fursa zaidi za kujikwamua kiuchumi,” amesema Waziri Soraga.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha amesema lengo la Mixx ni kuhakikisha huduma za kidijitali zinakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na si kurahisisha malipo pekee.

“Kwa mkulima wa mwani, tunataka teknolojia imsaidie katika maisha yake na shughuli zake za kiuchumi. Aweze kupokea fedha zake kwa usalama na kwa wakati, lakini pia apate huduma zinazoweza kumsaidia kuweka akiba, kupata mitaji na kukuza shughuli zake,” amesema Pesha.

Amesema, kupitia huduma kama Kilimo Pesa na Mixx Kikoba, wakulima wa mwani watapata fursa ya kutumia huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia kukuza shughuli zao na kuimarisha hali zao za kifedha.Mbali na sekta ya mwani, ushirikiano huo pia utasaidia utekelezaji wa programu nyingine za Zanzibar Maisha Bora Foundation.

Mixx itawezesha huduma za kidijitali katika Mariam Mwinyi Walkathon, ikiwemo usajili, malipo na uchangishaji wa fedha, pamoja na kuangalia namna teknolojia itakavyosaidia programu za afya kama Afya Bora Medical Camps.

Aidha, Mixx imechangia Shilingi milioni 350 kwa ajili ya bima ya wakulima kwa kipindi cha miaka mitatu na mwaka 2026 imetoa miche 25,000 ya mikarafuu bila malipo kwa wakulima Zanzibar.

Naye, Afisa Mkuu wa Yas Business, Norman Kiondo, amesema Yas Business itatumia uwezo wake katika mawasiliano na teknolojia kusaidia ZMBF kurahisisha utekelezaji wa programu zake na kuwafikia wananchi wengi zaidi Zanzibar.

“Kwa upande wa Yas Business, tunataka teknolojia iwe sehemu ya kutatua changamoto halisi,” amesema.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Rehema Tukai, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi, hususan wanawake na vijana wanaojishughulisha na kilimo cha mwani.