
Na Moses Ng’wat, Mbozi.
Wakazi zaidi ya 66,000 katika Mji Mdogo wa Mlowo, Kata ya Mlowo wilayani Mbozi, wameanza kunufaika na huduma za afya kufuatia kuanza kufanya kazi kwa Kituo cha Afya cha kata hiyo kilichojengwa na Serikali kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 63.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, aliyemwakilisha Mkuu w Mkoa katika maadhimisho hayo, alisema kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.
Amesema kituo hicho ambacho kilifunguliwa rasmi mwezi Machi mwaka huu na tayari kimeanza kutoa huduma za msingi, huku jitihada za kukamilisha miundombinu na huduma zikiendelea.

Mbega alieleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutaiwezesha jamii kupata huduma zote muhimu zikiwemo za mama na mtoto, uzazi pamoja na upasuaji bila kusafiri umbali mrefu.
Mkazi wa Mlowo, Andrea Shula, aliipongeza Serikali kwa kuanzisha huduma hiyo, lakini alisisitiza haja ya kuongeza wataalamu na huduma zaidi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Naye Elina Mgovana, mkazi wa Mtaa wa Forest, alisema kituo hicho kitapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya wananchi, hususan akina mama wajawazito waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya..

Akizungumzia umuhimu wa Muungano, Mbega alihimiza wananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano, akieleza kuwa misingi hiyo ndiyo chachu ya maendeleo ya Taifa.
Zoezi la usafi wa mazingira na upandaji miti lililofanyika katika kituo hicho ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano, likilenga kuboresha mazingira ya utoaji huduma za afya kwa wagonjwa na wahudumu.

More Stories
Wahimizwa kutumia zahanati ya Polisi Mabatini
Ilemela asilimia 100 kidato cha kwanza waripoti shuleni
Uwekezaji kwa wavulana kujenga uanaume imara