December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi Mecco wahakikishiwa kero ya maji kuwa historia

Na Judith Ferdinand,Timesmajira Online, Mwanza

WAKAZI wa Kata ya Mecco wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza, wamehakikishiwa hadi kufikia Septemba mwaka huu kero ya maji wilayani humo itakua historia.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Mecco, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya Kata kwa Kata wilayani humo ya kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19, kusikiliza kero na changamoto za wananchi na kisha kuzipatia ufumbuzi.

Masalla amesema, anatambua wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji ya uhakika hasa maeneo ya milimani na yenye sura ya vijiji.

Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan imekwishatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji, ambao Mbio Maalumu za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu zimeweka jiwe la msingi, hivyo Septemba mwaka huu mradi huo utakuwa umekamilika.

Pia amesema, baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa inayotekelezwa wilayani humo ukiwemo wa ujenzi wa tanki la maji uliopo mlima wa Kwa Mkuu wa Wilaya Kata ya Buswelu, unaogharimu zaidi ya sh. bilioni tano shida ya maji ndani ya wilaya hiyo itakuwa historia.

“Ni wahakikishe tu Wanamecco na wilaya kwa ujumla, kufikia Septemba shida ya maji itakuwa imekwisha kama si kupungua kwa kiasi kikubwa, sisi hatuwezi kukaa ofisini kama wananchi hamna maji wakati dhamira ya Serikali na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kumtua mama ndoo kichwani,” amesema.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Josephat Ilunde amesema jiji hilo linahitaji lita milioni 150 za maji, wakati uwezo wa kuzalisha kwa sasa ni lita milioni 90.

Mhandisi Ilunde, amesema hivyo upungufu uliopo ni lita milioni 60 ambazo zitapatikana baada ya kukamilika kwa chanzo cha maji Butimba kinachogharimu zaidi ya sh. bilioni 77 na kukamilika kwa miradi mingine inayoendelea ndani ya Wilaya ya Ilemela.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Shukran Kyando mbali na kuahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Wilaya alizitaka Mamlaka za Kata ya Mecco, kuheshimu mipaka ya kata hiyo iliyotangazwa mara ya mwisho katika Gazeti la Serikali.