April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAMWA yataka wanawake watayarishwe kabla ya Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Onlini, Zanzibar

VYAMA vya siasa nchini, vimeshauriwa kuwatayarisha wanawake katika nafasi ya uongozi kabla ya kufikia kipindi cha Uchaguzi Mkuu, ili waweze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Ushauri huo umetolewa na Wajumbe wa Kamati ya Wanaume wa Mabadiliko katika kikao cha pamoja na Maofisa wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) kilichofanyika Tunguu mjini hapa kutathmini hali ya ushiriki wa wanawake katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Wanaume zaidi ya 22 kutoka Unguja na Pemba, wakiwemo wafuasi wa vyama mbalimbali, wataalamu wa masuala ya jinsia na viongozi wa dini wameanzisha mtandao miaka mitatu iliyopita, ili kuhamasisha jamii kumpokea mwanamke kama kiongozi halali kama walivyo wanaume.

Mwenyekiti wa Kamati ya Wanaume wa Mabadiliko, Mohammed Jabir Makame amesema mifumo mibaya ya vyama vya siasa, inasababisha wanawake kushindwa majimboni kutokana na kutowatayarisha mapema kwa kuwapa nafasi ya kuongoza ndani vyama wanavyovipigania.

“Wanawake wanapewa nafasi ya kugombea jimbo wakati wa Uchaguzi Mkuu, bila ya kumtayarisha kwanza ndani ya chama chake hivyo si rahisi kushinda jimboni, ili kuona wanafanikiwa ni vyema chama kikamtayarisha kwa kipindi cha miaka minne nyuma kabla ya kufika Uchaguzi Mkuu kwa kumpa nafasi ya kuongoza ndani ya chama chake,” amesema.

Amesema awali wanawake walikuwa na woga wa kugombea nafasi ya majimboni lakini baada ya kuhamasishwa, wengi walijitokeza kugombea ambapo wanawake 435 walitia nia na 216 waligombea.

Kwa upande wake, Omar Mjaka Ali kutoka Pemba amesema mbali na utayari wa wanawake lakini pia wamekabiliwa na kikwazo cha kiuchumi, hivyo kinasababisha kukosa kushinda nafasi za majimboni.

Hata hivyo wanaume wa mabadiliko, wamesema wamejifunza mengi kutokana na harakati hizo za kutoa elimu kwa jamii kumkubali mwanamke kuwa kiongozi ikiwemo ulinganisho wa sheria, Quran na hadithi za dini ya Kiislamu.

Wamesema katika juhudi hizo, walikua wakitembea na viongozi wa dini ili jamii ifahamu kwamba dini ya Kiislamu haikukataza mwanamke asiwe kiongozi.

Takwimu zinaeleza kuwa hadi sasa, wanawake katika vyombo vya maamuzi hasa kupitia nafasi za kugombea ni wachache kwa mujibu wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020; Udiwani 25 sawa na asilimia 22.7, Baraza la Wawakilishi nane sawa na asilimia 16, Ubunge ni wanne sawa na asilimia 8 na Urais asilimia 0.

Pia wameiomba TAMWA ZNZ na wadau wengine kuendelea kutoa fursa za kuwajengea uwezo wanawake, vijana wa kike na kuwapa hamasa kuingia katika uongozi pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii, imkubali mwanamke kwamba anaweza kuongoza na dini si kikwazo cha kumzuia asiwe Mbunge, Mwakilishi wala Diwani.

Wanaume wa mabadiliko walifanya kazi kupitia Mpango wa Kuwainua Wanawake katika Siasa na Uongozi (WPEL), unaosimamiwa na TAMWA ZNZ kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na mambo ya wanawake (UN Women).