May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahitimu kidato cha 6 watakiwa kuripoti JTK

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

Kaimu Mkuu wa Utawala wa JKT Kanali Hassan Mabena

VIJANA waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita kwa mwaka 2021 wametakiwa kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria kuanzia Juni Mosi hadi 10 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkuu wa Utawala wa JKT, Kanali Hassan Mabena (pichani) amesema jeshi hilo tayari limewapangia makambi vijana hao katika kambi za JKT Rwamkoma Mara, JKT Msange Tabora, JKT Ruvu Pwani, JKT Mpwapwa, Makutupora JKT Dodoma, JKT Mafinga Iringa na JKT Mlale Ruvuma.

Kambi nyingine walizopangiwa vijana hao ni JKT Itaka Songwe, JKT Luwa, JKT Milundikwa Rukwa , JKT Nachingwea Lindi na JKT Kibiti Pwani na Oljoro JKT Arusha, JKT Mgambo, JKT Maramba Tanga, JKT Makuyuni Arusha , JKT Bulombora na JKT Mtabila Kigoma.

Aidha amesema wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho waripoti katika kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo .

“JKT inawataka vijana wote kuripoti wakiwa na vifaa mbalimbali ikiwemo bukta ya dark bluu,fulana ya kijani,raba za michezo rangi ya kijani au bluu,shuka mbili za kulalia rangi ya bluu bahari,soksi ndefu nyeusi ,nguo za kuzuia baridi,tracksuti yakijano au blui na nauli ya kwenda makambini na kurudi nyumbani.”amesema Kanali Mabena

Kanali Mabena kwa niaba ya Mkuu wa JKT Brigedia Jenerali Rajabu Mabele anawakaribisha vijana wote walioitwa kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia taifa.